JE NI KWELI MEDIA ZA DODOMA HAZITOI SUPPORT KWA WASANII WA NYUMBANI ?

Mazungumzo yangu na mmoja wa washkaji zangu nilipomuuliza, je ni kweli media za dom hazisapoti wasanii wa home? akaniambia hawajui namna ya kum-brand msanii, kumfanya aonekane special na akae midomoni mwa watu.
Tukubaliane kuwa zoezi la kufanya Branding kwa msanii linahusisha pande zote mbili yaani msanii na Media. Msanii ndiye mtu wa kwanza kufanya branding ya jina na kazi yake yeye mwenyewe kwa asilimia 50 ili sasa anapokwenda kwenye media inamalizia asilimia 50 zilizobaki. Brand yoyote inayojitengeneza yenyewe kwanza hufuatwa na waandishi wa habari kutokana na kuoneka kuwa ni hitaji la wasikilizaji, ndio maana utaona TMZ wakifuatilia watu maarufu mpaka vyumbani kwao. Ni lazima msanii aoneshe ile nia ya kuwa yeye ni brand kwa media, ni wazi wasanii wengi wa Dodoma kwa kupitia tafiti yangu , uzoefu na ukaribu wangu na tasnia changa kabisa ya muziki wa dodoma, nimegundua wengi hutaka kwenda studio kurekodi, kupewa interview nyimbo zao kuchezwa radioni kisha wiki mbili zijazo atarudi tena na wimbo mwingine radioni. Ndio maana utaona baadhi yao wakilalamika "radio hazichezi nyimbo au hazitoi sapoti kwa wasanii wa dom"
Ikumbukwe kuwa Radio karibu zote za Dodoma hutoa muda maalum kwaajili ya wasanii wa Dodoma tu. Je hii sio support? Kama kuna support nyingine kuna msanii yeyote au mdau aliyeandika maoni kupitia sanduku la posta la radio husika au kuifikisha barua yenye ombi au ushauri wa support gani wasanii wanahitaji kutoka kwenye vituo husika vya radio?
Ni wazi kuwa akili ya kila mmoja wetu inafikiria au kutamani kuona wasanii wa Dodoma wakijaza uwanja wa Jamhuri au japo kujaza clubs kama walivyo wasanii wengine wakubwa ambao tunashuhudia wakija na kuchukua hela zao pale maisha club, 84,Matei Lounge na kwingineko. Hakika hilo limekuwa gumu kwa kiasi fulani, je tunalaumu media pia?
Kuna upande mmoja ambao tunausahau sana, ambao ni sehemu muhimu sana kuliko chochote katika jambo hili. upande wa MASHABIKI au WAPENZI WA MUZIKI au tuseme WATU. hawa ndio lengo la muziki wetu lakini kama tunawsahau hivi. Je watu wanaridhishwa na kazi za wasanii? na wapo tayari kuwaunga mkono wasanii? Nina uhakika kabisa watu wanatambua kuwa Dodoma kuna wasanii , uhakika wangu unatokana na Media kuendelea kuishi ambapo inaonesha wazi watu wanasikiliza. Kama watu wangekuwa hawasikilizi radio za Dodoma basi hakuna radio hata moja ingeendelea kuishi mkoani Dodoma, zote zingekufa. Lakini kwa kigezo radio bado zinapiga mzigo inamaanisha kuwa kuna wengi wanaosikiliza, ndio maana wasanii wetu wanaweza kwenda nje ya Dodoma mjini na kufanya matamasha kwa hii hii promo ya radio zinazosemwa kuwa hazitoi support kwa wasanii wa nyumbani. Muulize Ainea, One Six, Zayumba na wengine wengi waliowahi kwenda kufanya matamasha sehemu za huko, Slimsal aliwahi kwenda Kondoa miaka mitatu iliyopita. Centrozone walipiga show pale Maisha Club,
Inawezekana labda wakazi wa mkoa wa Dodoma wamekosa uzalendo kwa wasanii au labda wasanii wa Dodoma hawajawapa mashabiki kitu wanachotaka au hawana kitu kabisa. Moja kati ya haya linaweza kuwa jibu sahihi. Lakini ningependa kutoa wito kwa wasanii kuzishawishi media kwa kutoa mikakati ambayo wanadhani itasaidia zaidi maendeleo ya muziki wao, na hata media pia iangalie uwezekano wa PLAN B ambayo inaweza kuwa na manufaa kwa pande zote mbili.

No comments

Powered by Blogger.