MFUMUKO WA BEI WAONGEZEKA NCHINI TANZANIA

Dar es Salaam. Mfumuko wa bei umeongezeka na kufikia asilimia 6.4 kutoka mwezi uliopita tofauti na ilivyokuwa Juni asilimia 6.1. Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraimu Kwesigabo alisema jana kuwa mfumuko huo umesababishwa na ongezeko la bei za bidhaa mbalimbali ikiwamo chakula. Kwesigabo alisema bidhaa za vyakula na vinywaji zimeongezeka kutoka asilimia 10.1  hadi 10.6 kulinganisha na Juni. “Mfumuko wa bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapimwa kwa kiwango cha badiliko la kasi ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi,” alisema. 
Alisema bidhaa zilizosababisha ongezeko hilo ni mchele ulioongezeka kwa asilimia 27.9, mahindi (2.3), unga wa muhogo (9.2), nyama (4.5), samaki (12.2), vyakula kwenye mgahawa (5.8) na maharage (5.9). Alisema mavazi ya kiume yameongezeka kwa asilimia 8.6, nguo za kike (6.5), huduma za malazi (3.7), cherahani (3.8), gesi ya kupikia (3.7), dizeli (5.9) na petroli (4.9). Kwesigabo alisema hali ya mfumuko wa bei nchini unamwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki. “Uganda mfumuko wa bei umeongezeka hadi asilimia 5.4 kutoka 4.9 ya Juni, huku  Kenya ikishuka mpaka asilimia 6.62 kutoka 7.03,” alisema Kwesigabo.


By Emma Kalalu na Florid Mapunda, Mwananchi.

No comments

Powered by Blogger.