MAKOSA MAKUBWA YANAYOFANYWA KWENYE VIDEO ZA MUZIKI ZA WASANII WA TANZANIA
Katika makala hii usipokuwa makini kidogo unaweza kudhani sipendi music videos nzuri au za gharama, lahasha,napenda video nzuri. Naandika makala hii ili tujadili kuhusu muziki wetu usonge mbele zaidi. Nina mambo matatu ambayo naona ni changamoto katika muziki wa Tanzania au Bongo Flava.
La kwanza, ni kuomba wanamuziki kuwa makini na muziki kuliko music videos. Nilichogundua mimi ni kuwa sasa hivi wanamuziki wanaumiza vichwa zaidi katika video itakuaje kuliko muziki wake na hii ni hatari kubwa sana na ukubwa wa hatari hii ni kwa kuwa muziki unaweza kupotea(kufa) kimya kimya bila watu kujua kama muziki unakufa, kufumba na kufumbua haupo. Mbaya zaidi kuna style music video ndio inaanza kutoka. Mwanamuziki akubali akatae kazi yake si filamu ni muziki kwa mantiki hii aumize kichwa sana kwenye muziki kuliko video, akiumiza kichwa kwenye video kuliko muziki nakosa kundi la kumweka.
La pili, muziki ni kitambulisho katika mambo tofauti tofauti mengi, nchi inatakiwa kumsupport mwanamuziki katika mambo mengi kama haki miliki ili anufaike na kazi yake. Nchi pia kupitia wananchi imsaidie mwanamuziki kwa kununua kazi zake, kumpigia kura kwenye tuzo mbalimbali ili akatambulishe taifa. Ila mwanamuziki pia anatakiwa atambulishe taifa. Kuna njia nyingi za mwanamuziki kutambulisha taifa ila mi ntazungumzia upande wa music videos. Huu mchezo wa kila mtu kwenda kushuti videos South Africa umeanza kukera sasa. Hatari yake tutaanza kuyalaumu mataifa yatakayoanza kuwataja wanamuziki wetu kuwa ni wa kwao. Kuna nchi ilishasema mlima Kilimanjaro ni wao tukalaumu sana bila kuangalia tulibugi wapi,wao wanahangaika kwenda nchi tofauti kutangaza si tumezubaa kazi kulalamika. Kuna nchi kubwa Afrika imewahi kuwa ikitangaza Ulaya kuwa Kilimanjaro upo masaa matatu kutoka airport yao badala ya kutaja nchi ulipo mlima huo.Kuna mambo matatu ya utetezi wanayozungumzia wanamuziki kuhusu kwenda nje kushuti videos zao, (1)ubora(2)mazingira(3)connection za TV kubwa. Siwezi kupoteza muda mrefu kujadili mambo mepesi kama haya. Ubora wa video asilimia kubwa ni camera na lens(hasa lens)na editing. Hawa wanamuziki kila siku kwenye kazi zao wanakutana na wafanya biashara wenye uwezo, wao na madirector wa videos wanashindwa nini kushawishi wafanya biashara hao kuweka hela kwenye productions, sio hela ya kutisha sana. Connections nasikia uvivu hata kuzungumzia -connections zinatengenezwa jamani? Fanyeni meetings za mara kwa mara na directors wa video nchini jinsi ya kufanya haya mambo, haya mambo yanahitaji team ili kusonga. Suala la mazingira nalo naona uvivu, maana hao wenye nchi yenyewe mnayokimbilia wao videos zao hawaendi kwenye hayo maghorofa mnayokimbilia na nyumba za vioo,kama hukubaliani na mimi anza kufuatilia videos zao na wanafanya vizuri kimataifa.
Video ni concepts na story line nzuri. Hii itasababisha mtu analia kaachwa na mpenzi wake sababu ya umaskini huku yupo nyumba ya ghorofa ya vioo, kama haijatokea itakuja kutokea tu.Suala la tatu, wanamuziki wasikurupuke kwenye utayarishaji au niseme wasiwe wajuaji sana, maana wengi wao wakiambiwa watoe mawazo yao katika video wanahisi kuwa wameshakuwa ma director au kwakuwa wameshafanya videos kadhaa basi wanajua kila kitu. Director hiyo ndio kazi yake anajua zaidi ya wewe mwanamuziki, msikilize sana director usimforce, mwisho atakubali halafu utakuwa umeharibu. Mchangiane mawazo ila uwe msikivu sana kuliko kuongea. Nasema hivi maana nimeshawahi kuona music video mwanamuziki anaimba nyumba yake inauzwa lakini nyumba inaonekana muonekano wa kuwa kuna hatari imefanyika pale(crime scene) kwakuwa ina tape ya polisi kabisa ya ‘do not cross.’ Kulifanya kosa liwe kosa zaidi utepe wa do not cross wa polisi ni wa nchi nyingine. Mmiliki wa kampuni iliyoshuti video hiyo ambaye ndio director ni rafiki yangu miaka mingi nyuma ambapo alikuwa hafahamiki bado. Kwa kumfahamu kwangu nakataa kuwa yeye ndio aliyetoa idea hiyo au aliafiki kirahisi wazo hilo.
Video nyingine nimewahi kuona eti polisi anakuwa mlinzi katika library na kulifanya kosa liwe kosa zaidi analinda ndani ya library. Sehemu inayofahamika kwa ukimya na kutotaka movement zisizokuwa na umuhimu, haya makosa ni mengi kwenye videos nyingi. Kwa kumalizia videos nzuri ni muhimu sana kwenye muziki, lakini ikumbukwe biashara inayouzwa hapo ni muziki,video ni promotion na marketing strategy ya kuuza muziki. Mwanamuziki usipokuwa makini itakuwa kisengere nyuma.Ni mawazo yangu na ndio maana ikaitwa makala.
Leave a Comment