VIKONGWE MAJAMBAZI WALIOTIKISA DUNIA YA UHALIFU (Part 1)

Flying Squad, kitengo maalumu cha polisi nchini Uingereza ambacho kwa jina lingine kinajulikana kama SCD7 (Serious Crime Directorate 7) kitengo kinachohusika na uchunguzi wa matukio makubwa uhalifu na yaliyotumia weledi wa hali ya juu, kitengo hiki mpaka leo hii ikiwa inakaribia miaka miwili kiko katika msako mkali wa kumtafuta muhalifu wasiyemjua jina na wamembatiza jina la 'Basil'.

Basil anatafutwa kwa kupanga na kutekeleza tukio la ujambazi lililotumia weledi wa hali ya juu na moja ya matukio ya ujambazi yaliyo wezesha kuibiwa vitu vyenye thamani ya hali ya juu kabisa katika historia ya nchi ya Uingereza.

Tukio hili alilitekeleza na wenzake wapatao saba ambao wote wametambuliwa na kujulikana isipokuwa Basil pekee amabaye ndiye alikuwa kiongozi wa mpango huu (mastermind) hajajulikana ni nani (Identity) na wala hajajulikana anaishi wapi.

Kitu pekee kinachojulikana kuhusu Basil ni kwamba alikuwa na ufahamu wa hali ya juu na 'access' ya sehemu ambapo tukio hili lilikuwa linaenda kutekelezwa. Sehemu yenyewe ni Hatton Garden.


Katikakati ya jiji la London, upo mtaa unaitwa Hatton Garden. Hii ni moja kati ya sehemu yenye utajiri mkubwa duniani kutokana na kuwa na moja kati ya mitaa duniani inayoongoza kwa biashara ya madini na Vito vya thamani. Huu ndio mtaa unaoongoza nchini Uingereza kwa kuwa na wauzaji na wanunuzi wengi wa almasi (diamond dealers) na madini mengine yenye thamani kubwa kama dhahabu na platinum.

Katika mtaa huu ipo kampuni maarufu inayomiliki kuba kadhaa (vaults) kwa ajili ya wafanya biashara kuhifadhi vitu vyao vya thamani hasa madini ya almasi na dhahabu. Kampuni hii inajulikana kama Hatton Garden Safe Deposits Ltd. Moja ya vault za kampuni hii yenye kutumiwa sana na wafanyabiashara iko jengo namba 89-90, ambalo ni jengo lenye ghorofa saba na vault yenyewe iko chini kabisa ya jengo (basement).

Vault hii inapendewa kutumiwa na wafanyabiashara wengi katika mtaa wa Hatton Garden kutokana na usalama wake wa hali ya juu. Kama nilivyoeleza, Jengo hili lina ghorofa saba. Katika Jengo hili kuna wapangaji wengine wapatao 60 ambao wengi wao ni wafanya biashatmra za madini. Vault yenyewe iko chini ya jengo.

Mbele ya jengo kuna mlango wa kuingilia. Mlango huu unatumia funguo kufungua na kufunga. Kila mpangaji kwenye jengo hili ana ufunguo mmoja wa kumuwezesha kufungua mlango huu. Pia ukishafungua mlango huu unakutana na mlango mwingine wa kioo ambao unafunguliwa kwa kutumia neno la siri (PIN code) ambayo wapangaji wote ndani ya jengo wanayo. 


Baada ya hapo unakutana na lifti kwaajili ya kumpeleka mtu floor ambayo makazi yake yapo. Lakini lifti hii imetengenezwa katika namna kwamba haishuki mpaka chini kwenye 'basement' ya jengo. Yani kwamba, mtu anaweza kutumia lifti kupanda nayo juu kwenda kwenye floor yeyote na pia anaweza kushuka nayo kutoka juu mpaka ghorofa ya chini (ground floor) lakini lifti haiwezi kushuka kwenda chini ya jengo, yaani kwenye basement. (Kumbuka vault ipo huko chini kwenye basement).
Pembeni ya lifti kuna mlango ambao ukiufungua unakutana na ngazi zinazoshuka chini kwenda kwenye basement. Mlango huu unafunguliwa kwa funguo maalumu ambayo moja anakuwa nayo mtu kutoka kampuni ya ulinzi ya H.G.S.D na funguo moja anayo mtu wa usafi pekee.

Ukishachuka chini kwenye ngazi na kufika chini kwenye basement mkono wa kushoto unakutana na mlango mwingine ambao unatumia funguo maalumu ambayo anakuwa nayo mlinzi wa H.G.S.D pekee. Ukishafungua mlango huu unakuwa na sekunde 60 kuingiza tarakimu za siri katika keypad iliyoko ukutani ili kuzima (deactivation) alamu ya tahadhari (intruder alert). Alarm hii inakaa kimya kwa sekunde 60 pekee na kama tarakimu hizo za siri hazitoingizwa kwenye keypad iliyoko ukutani, basi itapiga kelele na pia kutuma ujumbe maalumu wa simu kwa jeshi la polisi la London.

Baada ya kufungua mlango huu kuna geti dogo la chuma ambalo linafunguliwa kwa kutumia namba za siri (PIN code) alafu unakutana na kichumba kidogo cha mlizi ambapo pembeni yake kuna mlango mwingine wa chuma ambao huu unafunguliwa kwa kuusukuma tu kisha unakuwa uko mbele ya mlango wa Vault yenyewe.

Vault yenyewe inafunguliwa kwa kuingiza namba kwa mpangilio maalumu (combination) na kisha kuzungusha ringi lake. Hapa unakuwa uko ndani ya vault yenye viboksi takribani 966 zenye madini, fedha taslimu, Vito vya thamani vyote hivi vikiwa na thamani ya mamia ya mabilioni. Hii ndio vault ambayo Basil alikuwa amepanga kuiba. Licha ya kiwango hiki kikubwa cha ulinzi na teknolojia hii kubwa ya ulinzi, lakini thamani kubwa ya 'mzigo' uliopo ndani ya vault ukamfanya Basil aweke mkakati wa kuiba vault hii.

The Team

Ili kufanikisha lengo hili aling'amua wazi kuwa hawezi kufanya tukio hili peke yake. Alihitaji wabobezi wengine wa kushirikiana nao ili kufanikisha kutengeneza mkakati wa kuiba katika hii vault.

Ndipo hapa akawasiliana na mzee wa miaka 76 aliyeitwa Brian Reader. Huyu alikuwa ni mwizi nguli mstaafu aliyekuwa na weledi wa hali ya juu kuhusu upangaji wa mikakati ya ujambazi.

Huyu alikuwa moja ya washiriki katika tukio la ujambazi la kihistoria la wizi wa Bank ya Lloyd tawi la London mwaka 1971. Tukio ambalo majambazi walichimba shimo chini kwa chini mpaka ndani ya bank na kuiba fedha na vitu vyenye thamani ya mabilioni.

Pia mzee brian aliwahi kushiriki tukio lingine kubwa mwaka 1983 la kuiba mzigo wa dhahabu iliyokuwa inasafirishwa uwanja wa ndege akishirikia a na jambazi maarufu jijini London aliyeitwa Kenny Noya.
Tukio hili lilimsababishia kufungwa miaka tisa jela na alipotoka ndipo akaamua "kustaafu" ujambazi.

Lakini Basil ambaye inakadiriwa anaweza kuwa na miaka 50, alimfuta mzee huyu na kumsisitiza juu ya mpango huo. Hasa hasa alikuwa akimgusia kuwa, anajua kama amestaafu lakini anaomba ashirikiane naye kufanya "Tukio Moja La Mwisho", litakalowaweka kwenye vitabu vya historia na pia kujipatia mabilioni ya kuwawezesha kuishi uzee mwema.

Baada ya takribani miezi miwili ya kunshawishi hatimaye mwezi February, 2015 Mzee Brian ambaye wenzake walipenda kumuita "The Old man" akakubali kushiriki kuandaa mkakati wa kufanikisha tukio hilo.

Na akamuweka wazi kuwa ili kufanikisha tukio hilo wanahitaji timu ya watu. Watu wenye weledi wa hali ya juu na uzoefu katika kufanya matukio makubwa ya ujambazi. Na akamueleza kuwa anataka awashawishi marafiki na wezi wenzake wa siku nyingi ili kufanikisha tukio hilo.

Ndipo hapa ambapo mzee Brian akawasiliana na wezi wenzake na ambao pia ni marafiki zake wa siku nyingi. Timu hii ambayo Mzee Brian aliitengeneza ilikuwa na watu wafuatao.

Terry Perkins, miaka 67. Huyu alikuwa ni moja ya wezi weledi kabisa katika jiji la london. Perkins anakumbukwa sana kwa ushiriki wake katika tukio la wizi kwenye gari la kusafirisha fedha la kampuni ya Security Express mwaka 1983 ambapo waliondoka na dola milioni 9.
Perkins alishiriki matukio mengine mengi ya ujambazi lakini tukio lililompeleka jela lilikuwa ni kitendo chake cha kumtishia kumteka na kumuua meneja wa benki aliyekuwa anamtakatishia fedha zake baada ya kuanza kumzunguka na kutaka kumtapeli.

Kitendo hiki kilimfanya Perkins kuhukumiwa miaka 22 gerezani, lakini akafanikiwa kutoroka gerezani na kwenda kuishi Hispania na kurejea Uingereza miaka 17 baadae akiwa amebadili jina.

Wa pili aliitwa Jones, miaka 60. Huyu alikuwa mwizi mzoefu na alichukulia wizi kama ni wito wake wa maisha (destiny). Jones alikuwa akitumia muda wake wote kujisomea kuhusu mbinu za wizi kwenye mitandao, namna ya kutoboa kuta za vault, namna ya kutoacha alama kwenye eneo la tukio (forensic evidence). Pia huyu ndiye alikuwa mtu mwenye nguvu zaidi za mwili na aliye fiti zaidi ya wenzake wote.

Watatu aliitwa Carl Wood, miaka 58. Huyu alikuwa ni mwizi nguli na alikuwa na weledi mkubwa wa kudili na 'system'. Carl mwenye umbo jembamba na mrefu hakuwa kama wezi wengine. Alijiweka kama mfanyabiashara muhimu. Alipendelea kuvaa suti kwa unadhifu mkubwa. Pia alikuwa na viongozi kadhaa wa jeshi la polisi amewaweka mfukoni.

Wanne aliitwa John Collins, miaka 75. Wenyewe walipenda kumuita "Kenny".
Huyu alikuwa ni "mwizi mjanja mjanja" ("mtoto wa mjini"). Alikuwa anaufahamu mkubwa ya mji wa London na watu wake. Mojawapo ya shughuli zake za 'kuzugia' ilikuwa ni kununua kwa watu saa za gharama na kisha anaenda kuziboresha kidogo na baada ya wiki kadhaa anawauzia wale wale waliomuuzia mwanzo pasipo wenyewe kujua.

Pamoja na hawa, Mzee Brian alifanikiwa kuwashawishi watu wawili wakiokuwa wafanyakazi kwenye jengo lenye Vault, akawashawishi wajiunge nao kwenye mpango huo.
Watu hawa walikuwa ni Hugh Doyle mwenye miaka 48 na William Lincoln mwenye miaka 60. Hawa walikuwa ni mafundi bomba katika jengo husika.

Sababu ya Mzee Brian Reader kuwashirikisha watu hawa kwenye mpango huu ilikuwa ni kuzingatia kwamba kwa kuwa wao ni wazew basi watu hawa wawili wahusike zaidi kubeba vifaa vya kwenda kufanyia kazi na kubeba "mzigo" pindi wakimaliza kazi.

Mpaka hapo timu ilikuwa imekamilika. Kwahiyo jumka timu hii ya wazee hawa ilikuwa na watu 8. Mzee Brian Reader ("The old man"), Mzee Perkins (aliyetorokaga jela kifungo cha miaka 22), Mzee Jones (yule mwenye kuamini wizi ni 'destiny' yake, Mzee Carl (yule nadhifu na mwenye connection kwenye 'system'), Mzee Collins "Kenny" (mjanja mjanja), pamoja na mafundi bomba wale wawili (Doyle na Lincoln), na mwenyewe Basil (the mastermind).

Mwezi mmoja baadae yaani March, 2015 wakaanza kusuka mikakati juu ya namna ya kuingia ndani ya vault pasipo kugunduliwa. Vikafanyika vikao usiku na mchana, zikatafutwa ramani za jengo husika. Zikatafutwa ratiba za shifti za walinzi wa jengo pamoja na taarifa teknolojia zote zinazotumika kulinda jengo hilo.



Itaendelea....
Mwandishi: The Bold

No comments

Powered by Blogger.