FAHAMU DALILI 7 KUWA UTAKUJA KUFANIKIWA
DALILI 7 KUWA UTAKUJA KUFANIKIWA
Kila mtu duniani anataka kufanikiwa. Ni jambo ambalo unaliona katika binadamu toka anapozaliwa. Utamuona mtoto mchanga atapojaribu kusimama mara kwa mara mpaka atapofanikiwa kufanya hivyo na utaona watu wazima wakihangaika huku na kule ili kuhakikisha wanapata mafanikio katika nyanja mbalimbali. Baada ya kufanya uchunguzi wa kina wa watu waliofanikiwa katika ujasiriamali, niligundua wengi wao wana vitu 7 ambavyo huwa tofauti na watu ambao hawajafanikiwa. Leo hii napenda tuangalie vitu hivi 7. Vitu hivi vinaweza kusemwa kuwa ni dalili za kuwa utakuja kufanikiwa iwapo utakuwa navyo.
1. USHINDANI WA HALI YA JUU
Kuna wale watu ambao hupenda kushinda. Inaweza ikawa umekutana na watu hawa katika maisha yako. Mtu huyu yupo tayari kufanya kazi usiku na mchana ili afanikiwe. Inaweza ikawa yule jamaa aliyekuwa anakesha akisoma ili tu aweze kushika nafasi ya kwanza darasani. Inaweza ikawa yule rafiki yako ambaye hujitutumua kuvaa vizuri na kujiremba ili pale atapofika katika sherehe flani basi awe kati ya wale waliopendeza kupita wote katika sherehe hiyo. Hizi zote ni dalili za ushindani. Jambo hili ni muhimu sana ili kufanikiwa kwa sababu safari kuelekea mafanikio si rahisi. Mtu anayependa kushinda atatafuta njia ya kibunifu kuwashinda washindani katika biashara. Mtu anayependa kushinda hatokata tamaa kirahisi anapokutana na misukosuko na hivyo ana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa.
2. KUWA NA TABIA YA KUMALIZA VITU
Hapa ninaongelea uwezo wa kuanzisha jambo na kulisimamia mpaka unapofikia malengo. Watu wenye tabia hii hawaachi vitu nusunusu. Akisema anataka kupunguza kilo 20 atapigana mpaka kilo 20 zipotee. Akisema anataka kuanza kujenga nyumba mwakani atakazana mpaka ataposimamisha msingi hiyo mwakani. Akikuambia najifunza kiingereza basi atakomaa na English Course na baada ya miezi sita atakuwa anapiga ung’eng’e kama kazaliwa Marekani. Ni tabia muhimu sana kuwa nayo kwani ni dalili ya utayari wako wa kufanya kazi kwa bidii mpaka utapofika malengo yako. Na ukweli ni kwamba unahitaji kufanya kazi kwa bidii kwelikweli ili ufanikiwe katika ujasiriamali.
3. WATU WANAOKUZUNGUKA WANA KIPATO ZAIDI YAKO
Kwa wengi marafiki zao wa karibu huwa hawana tofauti na wao. Utakuta wamesoma shule zinazofanana, wanafanya kazi zinazofanana na wana vipato ambavyo havitofautiani sana. Ila kwa yule ambaye anapigana kufanikiwa utaona tofauti. Atajaribu kujihusisha na watu wenye kipato zaidi yake aidha moja kwa moja kwa kujuana nao na kuwa marafiki nao au kupitia vitabu na njia nyingine za mafunzo. Hili ni jambo muhimu sana kwani hutakuja kuweza kuogelea kama hutaingia katika maji. Unapojihusisha na watu ambao wamekuzidi mafanikio unajenga fursa kujifunza kutoka kwao lakini pia unapata motisha ya kuendelea kusonga mbele ili siku moja uweze kufikia levo yao ya mafanikio au zaidi. Iwapo unataka kufanikiwa hili ni jambo muhimu sana kuzingatia.
4. AKILI ZAO HAZISIMAMI
Ninaposema akili kutosimama ninamaanisha ni kuwa na mawazo ya jinsi ya kujiendeleza kibiashara muda wote. Ukiwa unakula unafikiria jinsi ya kupunguza matumizi katika eneo flani. Ukiwa unaoga unafikiria kuongea na mtu flani akupe tenda ya biashara. Ukiwa kwenye foleni Ubungo kichwani mwako unafikiria bidhaa mpya unaweza kuleta kutoka China. Ni akili zinazofanya kazi muda wote ndizo zinaweza kufika mbali katika ujasiriamali. Kuwa na jambo hili linaonesha kuwa wewe ni mbunifu na ubunifu ni jambo la muhimu sana ili kujenga biashara inayoingiza faida. Ubunifu utakuwezesha kutatua changamoto zitazokukabili katika safari yako kuelekea mafanikio. Akili yako kamwe isisimame.
5. WATU WANAKUONA UNAZIDI KUWA BORA SIKU HADI SIKU
Ninavyosema watu ninamaanisha wale wanaokuzunguka katika maeneo muhimu ya kikazi kama walimu na mabosi zako. Simaanishi familia yako au ndugu zako. Sifa kutoka kwa ndugu japokuwa ni nzuri, mara nyingi huwa ni za kukutia moyo na sio halisi kwa asilimia 100. Ila mwalimu au bosi wako anapokuambia una ufanisi mzuri wa kazi ni jambo tofauti. Hili pia ni kweli kama sifa zinatoka kwa mtu anayeheshimika katika sekta flani. Unapopata sifa kutoka kwa watu hawa inamaanisha unasogea karibu na mafanikio makubwa kadri siku zinavyoenda. Sifa hizi mara nyingine zinaweza kuja katika mfumo wa tuzo ziwe ndogo au kubwa. Endelea kukaza mwendo na utapata mafanikio makubwa zaidi.
6. UNAJIFUNZA MUDA WOTE
Kuna yule rafiki yako anayependa kusoma vitabu sana. Kuna yule mwingine anayependa kwenda kwenye semina za mafunzo ya ujasiriamali kila akipata fursa hiyo. Kuwa wale wengine ambao wanapoona tu kitu flani hawakijui basi huwa na haraka kuwatafuta wale wanaokifahamu kitu hiko ili wajifunze kutoka kwao. Hii ni tabia muhimu sana katika safari kuelekea mafanikio kibiashara kwa sababu mambo hubadilika. Leo njia hii ya kuingiza pesa inaweza ikawa inafanya kazi ila kesho njia hiyohiyo inaweza isikuingizie chochote. Mara nyingine unataka kupata mauzo zaidi unahitaji ujifunze njia mpya ya kujitangaza. Au unataka kukuza biashara yako kwa kuuza aina mpya ya bidhaa hivyo inabidi ujifunze mlolongo wa jinsi bidhaa hiyo inavyozalishwa hadi inapokuwa tayari kwa ajili ya kuuzwa. Bila kujifunza vitu vipya kila mara unakosa uwezo wa kubadilika pale inapobidi na kwa namna hii unaongeza uwezekano wa biashara yako kushindwa. Mtu anayejifunza muda wote atafanikiwa kirahisi zaidi na atapata mafanikio makubwa zaidi akiweka bidii katika shughuli zake.
7. KUKAMIA NA KUWA NA NJAA YA KITU KWA ASILIMIA MIA MOJA
Christiano Ronaldo ni moja kati ya wachezaji bora wa mpira wa miguu kuwahi kutokea katika historia ya dunia. Toka alivyokuwa mdogo sana alikua akicheza mpira kila siku. Alikuwa tayari kuchelewa kurudi nyumbani baada ya shule au kuacha shule kabisa kwa ajili ya mapenzi na mpira wa miguu. Mpira wa miguu kwake ulikuwa muhimu kuliko hata kula. Alivyokuwa mtu mzima hili halikubadilika. Ronaldo ndiye mchezaji anayefanya mazoezi kupita mtu yoyote katika timu zote alizochezea. Ukisema jamaa amekamia kufanikiwa unakuwa hujakosea. Na leo hii amefikia mafanikio aliyokuwa anayatamani lakini bado anaendelea na bidii ileile. Ni hamu hii nzito ya kufika juu inayotofautisha waliofanikiwa na wanaoshindwa. Inabidi kuwa na njaa isiyotingishika ya mafanikio. Katika safari yako kuna watakaokusema, kuna watakaokutapeli na kuna watakaokutakia mabaya. Ila kama umekamia jambo, kama una njaa haswahaswa ya kufanikiwa vitu hivyo vyote vitakuwa kama upepo tu na havitakurudisha nyuma kwa namna yoyote. Utaendelea kusonga mbele mpaka utapofikia malengo yako.
Dalili hizi 7 si kuwa mtu anazaliwa nazo. Hizi ni tabia ambazo mtu yeyote anaweza kuwa nazo. Mambo haya mtu yeyote anaweza kujifunza na yakamsaidia kufikia mafanikio. Jifanyie tathmini na jitambue ulivyonavyo. Kwa ambavyo huna basi anza kuvijenga sasa. Kwa ambavyo unavyo jitahidi uvikuze zaidi na zaidi kwani unapokuwa bora zaidi katika mambo haya ndivyo itavyokuwa rahisi zaidi wewe kufikia mafanikio makubwa katika ujasiriamali na kwingineko maishani.
Leave a Comment