LUCKY DUBE: MIAKA KUMI (10) TANGU AUWAWE
Dube aliyeuwawa akiwa na umri wa miaka 43, alizaliwa sehemu inayojulikana kama Ermelo, Transvaal (kwa sasa Mpumalanga) mwaka 1964, Augusti, 3. Wazazi wake walitengana kabla ya kuzaliwa kwake na aliishi na mama yake ambaye alimpa jina la LUCKY kwa maana ya bahati; hii ni kutokana na mimba kadhaa kuharibika, hivyo kuzaliwa kwa Lucky Dube ilionekana kama ngekewa au bahati.
Pamoja na ndugu zake wawili Thandi na Patrick, Dube alitumia muda wake mwingi wa utotoni akiishi na bibi yake aliyejulikana kwa jina la Sarah wakati mama yake alipokwenda kazini. Mwaka 1999 kwenye moja ya interview yake, Dube alimuelezea bibi yake kama 'kipenzi chake kikubwa' ambaye alifanya kazi kubwa ya kumlea, na kumkuza Dube.
Kuanza Muziki
Katika umri wa utotoni, Dube alifanya kazi kama mtunza bustani na kadiri alipokuwa akikua, aligundua kuwa kipato alichokuwa akikipata hakikutosheleza kuilisha familia yake, ndipo Dube alianza shule. Katika mazingira ya shule alijiunga na kikundi cha muziki kilichoitwa The Skyway Band. Alijifunza na kufuata imani ya kirasta akiwa shule, na alipofikisha umri wa miaka 18 Dube alijiunga na kundi la muziki la binamu yake lililojulikana kwa jina la The Love Brothers, ambalo lilipiga muziki wa Kizulu aina ya mbaqanga. Akiwa na kundi hilo, waliweza kuingia mkataba na kampuni ya muziki Gallo Music, kampuni kubwa kabisa huko Afrika Kusini.
Dube, alivutiwa zaidi na muziki wa Jimmy Cliff na Peter Tosh toka Jamaica, na ndipo safari yake ya kuimba muziki wa reggae ilipoanzia. Mwaka 1984, alirekodi album yake ndogo ya reggae iliyokwenda kwa jina la Rastas Never Die, hata hivyo album hiyo haikufanya vizuri sokoni ambapo iliuza nakala 4000 (elfu nne) tu ukilinganisha na mauzo yaliyofanyika kwenye muziki wa mbaqanga ambapo aliuza hadi nakala 30,000 (elfu thelathini). Akiwa mwenye shauku kubwa ya kupiga vita ubaguzi wa rangi (ant-apartheid), kupitia muziki na tungo zake mbalimbali, serikali ya kibaguzi ya wakati huo ilipiga marufuku album yake mwaka 1985 kutokana na mashairi ambayo yalionekana kuikosoa serikali ya kibaguzi. Hakukata tamaa, kwani mwaka huo huo wa 1985 aliendelea kuimba muziki wa reggae na aliweza tena kurekodi album yake iliyoitwa Think About The Children iliyompa mafanikio makubwa kwa kuuza nakala na kufikia hadhi ya mauzo ya platinam na kumpaisha na kuwa moja ya wanamuziki maarufu zaidi huko Afrika Kusini na nje ya Afrika Kusini.
Dube aliendelea kutoa album za reggae ambapo mwaka 1989 alishinda tuzo ya OKTV kwa album ya Prisoner, tena akashinda tuzo kutokana na album ya Captured Live (iliyotokana na onesho la moja kwa moja). Mwaka uliofuata alitoa album ya House of Exile. Mwaka 1993 album yake ya Victims, iliuza zaidi ya nakala milioni moja duniani kote. Mwaka 1995 alipata mkataba wa kurekodi na Motown moja ya makampuni makubwa kabisa nchini Amerika, ambapo Trinity ndiyo album ya kwanza kurekoodiwa na kampuni hiyo. Dube inaaminika kuwa ndiye mwanamuziki bora zaidi toka Afrika kusini, na miongoni mwa wanamuziki wachache toka bara la Afrika kufanya vizuri katika soko la kimataifa. Pia kutokana na kukubalika hadi nje ya Afrika, moja ya wimbo wake unaojulikana kama Victims, toka album iliyobeba jina hilo VICTIMS, ulifanyiwa marudio (cover) na mwanamuziki wa reggae nchini Jamaika anayeitwa Anthony B.
Mwaka 1996, alitoa album mjumuisho iliyokwenda kwa jina la, Serious Reggae Business, ambayo ilifanya awe muuzaji bora na kutajwa kama mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa wakati wa utoaji wa tuzo za World Music Awards kadhalika kama mwanamuziki bora wa kimataifa kwenye tuzo za Ghana Music Awards. Album zake tatu zilizofuata zilifanya ashinde kwenye tuzo za South African Music Awards. Album yake ya hivi karibuni, Respect, ilisambazwa na kampuni ya Warner Music. Dube amezunguka dunia aki-perform na wanamuziki kama Sinéad O'Connor, Peter Gabriel, Celine Dion, Ziggy Marley na Sting. Mwaka 1991 aliweza kushirki tamasha kubwa zaidi la reggae sunsplash huko Jamaika ambapo aliombwa arudie tena kutokana na umahiri wake na upekee wa aina yake kama mwanamuziki toka barani Afrika.
Mnamo tarehe 18/10/2007, Lucky Dube aliuwawa jijini Johannesburg kwenye kitongoji cha Rosettenville muda mfupi baada ya kuwashusha watoto wake wawili karibu na nyumba ya ndugu yake. Dube alikuwa akiendesha gari yake ya kifahari aina ya Chrysler 300C, ambayo waporaji walikuwa wakiitaka. Wauaji hao, katika kujitetea, walidai hawakujua na kugundua kuwa aliyekuwa akiendesha gari hiyo alikuwa Lucky Dube bali walijua alikuwa ni Mnigeria. Watu watano walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo na walipatikana na hatia hivyo walihukumiwa kifungo cha maisha tarehe 31 Machi 2009. Wengine wawili walifanya jaribio la kutoroka lakini walikamatwa na wote wanatumikia kifungo cha maisha. Mtandao wa mwanamuziki maarufu toka Jamaika, na mfalme wa reggae duniani, hayati Robert Nesta Marley maarufu kama Bob Marley (www.bobmarley.com) pia ulihabarisha dunia juu ya kifo cha Lucky Dube miaka kumi (10) iliyopita, hii inatoka na jinsi alivyoheshimika hata huko Jamaika ambako reggae ndiyo asili yake.
Lucky Dube atakumbukwa zaidi kwa nyimbo zake kama vile, Together As One, Prisoner, Reggae Strong, Different Colours One People, Remember Me, My Brother My Enemy, Serious Reggae Business, Reggae Strong For Peace, God Bless The Women, Trinity, The Way It Is, Victims, na nyinginezo nyingi.
Leave a Comment