HISTORIA YA KWELI YA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA

KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA

SEHEMU YA KWANZA
“...kama unasoma ujumbe huu, muda huu… uko mpweke! Pengine ushahidi pekee uliobakia ni kijipande hiki cha maandishi. Sijui kama kuna yeyote kati yetu aliyesalimika kufika kizazi chenu mwaka huu mtakaosoma andishi langu. Sijui hata kama tumeshinda au tumeshindwa vita tunayopigana sasa hivi. Sijui, lakini naamini mwaka huu mliopo nyinyi sasa mwaweza kuwa na jibu sahihi. Vyovyote vile lakini jambo lililo dhahiri ni kwamba hakuna yeyote wa kizazi chetu mliye naye sasa hivi kwenye miaka yenu muusomapo ujumbe huu. Kwa hiyo wacha niwaeleze sisi tulikuwa akina nani, na kwa namna gani tulipambana mpaka tone la mwisho la damu mwilini mwetu ili kutetea kizazi chetu kisifutwe juu ya uso wa dunia. Wacha niwaeleze namna ambavyo japo tulikamuliwa damu mpaka kutiririka kufanya mifereji lakini lakini tulisimama kutetea kizazi chenu na ninyi watoto wetu. Wacha niwaeleze kisa kilichotikisa ulimwengu. Wacha niwaeleze kuhusu mifereji ya damu kwenda Ethiopia.!”

– Habib Anga alias The Bold

March 21, 1994 maeneo ya Uganda ambayo yanapakana na Rwanda, katika ziwa viktoria serikali ilituma vikosi vya jeshi kudhibiti eneo hilo kwa hali ya dharura. Agizo hili la serikali kutuma jeshi halikuwa kwa ajili ya kidhibiti eneo hilo kutoka kwa adui bali agizo lilikuwa ni kudhibiti eneo hilo dhidi ya maiti, maiti za binadamu. Sio maiti mbili au tatu, si mamia bali maelfu ya maiti za binadamu ambazo zilikuwa zinaingia ziwani Victoria zikiletwa na maji ya mto Kagera.

Maiti hizi zilikuwa nyingi kwa maelfu kiasi kwamba mapaka zilikuwa zinafanya maji yatoe harufu. Serikali ya Uganda ilituma jeshi eneo hili ili kudhibiti eneo hili maji yake yasitumiwe na wananchi kwa matumizi ya nyumbani au shughuli za uvuvi. Lakini jeshi lilikuwa eneo hili ili kuhakikisha kuwa taharuki iliyozuka baada ya maelfu ya miili hii kuonekana haigeuki na kuvuruga amanai katika eneo hili. Lakini pia jeshi lilikuwa hapa ili kubaini miili hii ilikuwa inatoka wapi.

Kadiri ambavyo jeshi la Uganda lilivyokuwa linafuatilia kwa kurudi nyuma kufuata mto Kagera ndivyo ambavyo walizidi kubaini kwamba maiti hizo zinaletwa na maji kutoka tawi la mto Kagera lililopita kusini mwa Rwanda. Na kadiri ambavyo walizidi kufuata chanzo cha maiti hizo zinakotoka ndivyo ambavyo walikuwa wanaikaribia Rwanda na maji ya mto rangi yake kuwa nyekundu zaidi.

Wanajeshi wa Uganda ambao walishiriki kwenye ukaguzi huu wa mto huu wanakiri kwamba licha ya baadhi yao kupigana mstari wa mbele kwenye vita mbali mbali lakini hakuna yeyote kati yao ambaye aliwahi kushuhudia ukatili mkubwa wa kiasi hiki.

Siku hii jeshi la Uganda linakisia kwamba waliokota si chini ya miili elfu kumi ya binadamu na yote ilionekana kuletwa na maji ya mto Kagera kutoka nchini Rwanda.
Ajabu ni kwamba miili yote hii ilikiwa inamfanano fulani. Maiti zote zilikuwa za watu warefu, wembamba, wenye nyuso ndefu na pua za kuchongoka. Haikuhitaji kufikiria sana kufahamu kuwa maiti hizi zilikuwa za watu wa kabila la Tusi (Tutsi).

Miezi kadhaa baadae ndipo ambapo jeshi la Uganda na ulimwengu wote walikuja kuelewa kwa nini maiti zilikuwa zinatupwa mto Kagera. Ni ujumbe gani ambao ulikuwa unajaribu kutumwa.

Kwamba Watusi nchini Rwanda walikuwa waapenda kujisifu kuwa mababu zao wana asili ya nchi ya Ethiopia. Kitendo hiki cha watesi wao kuwatupa mtoni, walikuwa wanawaua na wakiwa wanatupa maiti zao mto wanawaambia kwamba “wanawasafirisha warudi kwao Ethiopia ambako wamekuwa wakijisifu ndio asili yao.”

Sio kwamba jeshi la Uganda hawakuwa na taarifa juu ya hali tete iliyopo Rwanda kwa muda wa karibia wiki nzima iliyopita bali hawakujua kama hali hiyo tete ilikuwa ni ya kinyama kiasi hicho.

Wanajeshi hawa wa Uganda walikuwa wameshikwa na bumbuwazi na vihoro vilivyo wapasua mioyo kwa kuona miili hii elfu kumi ya binadamu isiyo na uhai. Kitu ambacho walikuwa hawakijua na hakuna ambaye alidhahania ni kwamba ndani ya siku mia moja zijazo ulimwengu ulikuwa unaenda kushuhudia moja ya tukio la kikatili zaidi tangu kuubwa kwa ulimwengu. Karibia maiti za binadamu milioni moja zikiwa zimetapakaa mitaani nchini Rwanda iking’ong’wa na nzi na kuliwa na mbwa.

GENESIS


Rwanda: Kabla ya Ukoloni
Asili rasmi kabisa ya watu wa kwanza kuishi katika eneo ambalo leo tubalitambua kama nchi ya Rwanda ni watu wa kabila la ‘Twa’ (Watwa). Kabila hili la wawindaji si la kibantu bali ni sehemu ya makabila yanayotambulika na wanahistoria kama ‘pygmy’ ambao sifa yao kuu ni ufupi. Mtu mzima anayetoka makabila ya namna hii anakadirwa kuwa na wastani wa urefu chini ya sentimita 150. Watwa waliishi Rwanda enzi za kale sana miaka ya 8000 BC na 3000 BC.

Kuanzia miaka ya 700 BC mpaka 1500 AD makabila ya Kibantu kutoka maeneo ya jirani yalianza kuhamia eneo hili.

Kuna nadharia mbali mbali kuhusu ni namna gani haswa makabila haya ya kibantu yalihamia hapa na baadae kupelekea kutokea Makabila ya sasa ya Wahutu na Watusi.

Nadharia ya kwanza inadai kwamba; Wahutu ndio walikuwa wa kwanza kuhamia eneo hili na kuanzisha shughuli za kilimo. Baadae watu wenye asili ya Ukushi (Watusi wa sasa) nao wakahamia kwenye eneo hili na kulitawala.

Nadharia ya Pili inadai kwamba; kuna uwezekano kwamba Watusi si wakushi bali ni wahamiaji tu kutoka maeneo ya jirani kipindi hicho cha kale ambao walihamia na kujichanganya na jamii waliyoikuta hapo (Wahutu) lakini wao walikuwa wafugaji. Chini ya nadharia hii inadai kwamba kuibuka kwa Wahutu na Watusi hakukutokana na kuwa na utofauti wa kinasaba au asili ya mababu bali ulitokana na utofauti wa kimadaraja/matabaka ya kijamii.
Tabaka la wale walio wa daraja la juu ambao walikuwa wafugaji walijitanabaisha kama Watusi wakati ambapo tabaka la chini ambao walikuwa wakulima walijitanabasha kama Wahutu.

Makabila haya yote matatu, Watwa, Wahutu na Watusi wanazungumza lugha moja na kwa wote kwa pamoja wanajulikana kama ‘Banyarwanda’.

Idadi ya watu ilipoongezeka katika eneo hili walianza kujitambua kupitia makundi madogo madogo yaliyoitwa ‘Ubwoko’ au ‘koo’ kwa kiswahili. Ilipofika katikati ya miaka ya 1700 koo nyingi ziliungana na kuunda ‘Falme’.
Moja ya Falme ambazo zilikuwa imara zaidi ulikuwa ni ‘Kingdom of Rwanda’ ambayo watawala wake wote walitokea katika koo ya Kitusi ya Nyiginya.

Ufalme huu ulifikia kileleni kipindi cha utawala wa Mfalme Kigeli Rwabugiri chini ya falsafa yake ya kujipanua na kuteka falme nyingine na kuzifanya sehemu ya Kingdom of Rwanda.

Chini ya Mfalme Rwabugiri alianzisha mfumi wa kiuchumi wa ‘ubuhake’ na baadae ‘uburetwa’.
Katika mifumo yote hii miwili, iliwanufaisha zaidi Watusi na kuwafanya Wahutu kama vijakazi wao kuwafanyia kazi za uzalishaji na kuwa askari vitani kwa ujira wa kupata fursa ya kumiliki mifugo na kutumia ardhi.

Watusi walipaa juu zaidi na kuwa raia daraja la kwanza ma Wahutu kubakia kuwa tabaka la chini kabisa ndani ya Kingdom of Rwanda.

Rwanda: Wakati wa Ukoloni

Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ulilitoa eneo hili kuwa koloni la nchi ya Ujerumani. Wajerumani walitawala eneo hili kwa kushirikiana na Mfalme na hivyo kuwapa wepesi wa kutawala koloni bila kuwa na askari wengi wa kijerumani ndani ya ardhi ya Rwanda. Yuhi V Musinga ndiye walikuwa Mfalme wa Rwanda kwa kipindi hiki na anakumbukwa zaidi kwa kuwapokea Wajerumani kwa mikono miwili.

Ikulu ya Mfalme wa Rwanda maeneo ya Nyanza


Wajerumani ndio walikuwa watu wa kwanza kuanza kuwapandikizia Watusi kasumba ya kuwa wao si Wabantu. Wakoloni wa Ujerumani ndio ambao walieneza propaganda kwa kuwafundisha Watusi kwamba kutokana na tafiti zao za kina wamegundua kwamba wao (Watusi) mababu zao wa kale walihamia eneo hilo kutokea Ethiopia. Hivyo wakawashawishi kuamini kwamba Watusi wana vinasaba vya ‘uzungu’ (Caucasian) na hivyo ni wao pekee ndani ya Rwanda walistahili kupata nafasi za ajira kusaidizana kazi na wazungu chini ya utawala huo wa Wajerumani.

Katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Ubelgiji iliziteka Rwanda na Burundi kutoka mikononi mwa Ujerumani na mwaka 1919 League Of Nations ilizifanya rasmi nchi hizo kuwa makoloni ya Ubelgiji.

Mwanzoni Wakoloni wa Ubelgiji walianza kuitawala Rwanda kwa mtindo ule ule wa kushirikiana na Ufalme lakini baadae wakajilimbikizia madaraka yote ya kutawala kama ambavyo walifanya kwenye koloni lao la Kongo.

Baadae wakaanza ‘kutaifisha’ mali za Wanyarwanda katika mfumo wa kufanana kabisa na mfumo wa asili wa uburetwa na walioathirika zaidi na kampeni hii ya utaifishaji walikuwa ni Wahutu.
Ardhi yao ilinyang’anywa… Mifugo ilitwaliwa na kuwafanya Wahutu kuwa si tu vijakazi wa Wakoloni bali pia vijakazi wa Watusi.

Mwanzoni mwa miaka ya 1930s Ubelgiji walifanya upanuazi mkubwa wa sekta ya Elimu, afya na ajira za umma. Lakini wanufaika wakuu walikuwa ni Watusi.

Mwaka 1935 Ubelgiji walifanya kitu ch a ajabu sana ambacho kilipanua zaidi mpasuko wa kijamii na kitabaka uliopo ndani ya Rwanda. Walianzisha mfumo wa raia wote kuwa na vitambulisho. Vitambulisho hivi viliwatambua raia wote katika makundi manne kulingana na makabila yao. Watwa, Wahutu, Watusi na Raia wa kuomba (Naturalised).

Kutokana na Watusi kuwa ndio raia wa daraja la kwanza na tabaka la juu huku Wahutu wakiwa ni watu hafifu wa kudharaulika nchini humo, ilifikia hatua Wahutu wenye mali au ushawishi walikuwa wanahonga fedha ili kupatiwa vitambulisho vya Kuonyesha ni Watusi na watawala hawakuwapa Utusi kamili bali waliwapa ‘utusi wa heshima’ (Honorary Tutsi).

Hadhi ya Wahutu wote iliendelea kushuka kwa kasi wakionekana ni kabila na kizazi cha “Washenzi” huku Watusi wakionekana ndicho kizazi cha “wastaarabu” na kabila lenye darja.

Lakini kuna suala ambalo lilifanyika mwanzoni likionekana kuwa na manufaa makubwa lakini kadiri siku zilivyokwenda lilianza kuwa kama mkuki mgongoni. Kanisa Katoliki.

Kanisa Katoliki lilikuwa limeenea sana nchini Rwanda na raia wake wengi wakiwa ni waumini wa kanisa hilo. Tukumbuke kwamba tangu kipindi hicho Wahutu ndio walikuwa idadi kubwa zaidi ya raia wote ndani ya Rwanda. Hii ilimaanisha pia kwamba waumini wengi wa kanisa Katoliki walikuwa ni Wahutu.

Kwa kiasi fulani ndani ya kanisa Katoliki mapadri na watawa wengine walikuwa wanajisikia hatia kuacha waumini wao kuwekwa kwenye kundi la kizazi cha “washenzi” na kudharaulika ndani ya jamii. Kwa hiyo zikaanza juhudi za makusudi za kanisa katoliki kutoa elimu kwa vijana wenye asili ya Kihutu.

Baada ya miaka kadhaa kukaanza kuwepo walau kidogo uwiano wa wasomi wa Kihutu na Kitusi.

Mwaka 1957, mwezi March kikundi cha wasomi na watu wenye ushawishi wenye asili ya Kihutu walifanya jambo la “kimapinduzi” ambalo lilipanda mbegu mpya kwenye nafsi za watu wa kabila na kizazi cha cha Kihutu. Waliandaa waraka ulioitwa _'Manifeste des Bahutu' (Bahutu Manifesto).
Huu ndio ulikuwa waraka wa kwanza rasmi kubainisha kwamba Wahutu na Watusi ni mbari (race) mbili tofauti.

Katika waraka huu, wasomi hawa na watu hawa wenye ushawishi walijenga hoja kuu kwamba… Watusi wanapaswa kutoka kwenye jukumu lao walilojivesha la kuwa watawala wa Rwanda na badala yake nafasi hiyo ya kutawala Rwanda wapewe Wahutu. Hoja yao hii waliijenga kwenye nadharia ambayo wenyewe waliita “Statistical Law”, kwamba kitakwimu Wahutu ni wengi mno kushinda Watusi. Si sawa wakiendelea kutawaliwa na kufanywa vijakazi na Watusi.

Wanasema kwamba kabla kibanda cha nyasi kuungua kwanza utaanza kukiona kinafuka moshi. Kuna vugu vugu lilianza chini kwa chini ndani ya Rwanda.

Waraka huu… Bahutu Manifesto, ulitoka tarehe 4 March mwaka 1957. Japokuwa ilikuwa ni miaka takribani 37 kabla ya mwaka 1994, lakini ndio siku ambayo mbegu ya mauaji ya kimbari ilipandwa.

Usikose sehemu inayofuata….

Itaendelea…

Chazo : Jamiiforums
Mwandishi: The Bold
To Infinity and Beyond.

Image result for animated download now gif

No comments

Powered by Blogger.