JANUARY MAKAMBA NA STORI YA SAFARI YA JAMAICA, ANAMAANISHA NINI HAPA?


Mwaka 2008, nilipata bahati ya kutembelea Roma, Italia. Nilitahidi kuzunguka karibu mji mzima kwa miguu na kwa teksi ili kuimeza kwa uhakika historia kubwa ya jiji hilo. 

Siku moja nilitumia nusu siku kutembelea Vatican, pamoja na maeneo yake muhimu ikiwemo Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro (St. Peter’s Basilica), nje ya Sistine Chapel na maduka rasmi ya Kanisa yanayouza bidhaa mbalimbali za kiroho/kanisa.

Ingawa mimi ni Muislam, nilinunua zawadi nyingi (rozari, skapulari, maji yaliyobarikiwa, n.k) kwa marafiki zangu Wakatoliki. Nilinunua rozari moja nzuri sana kwa rafiki yangu niliyekuwa nafanya naye kazi, ambaye pia ni Mkatoliki mzuri. Nilivyorudi kutoka safari bahati mbaya sikuweza kumpa zawadi yake ya rozari kwa sababu aidha tulikuwa tunapishana au nilikuwa naisahau nyumbani.

Siku moja wakati tunasafiri kwenda Jamaica pamoja nikampa zawadi yake ya rozari tukiwa tumekaa kwenye ndege. Akafurahi sana na kuniambia kwamba aina ile ya rozari niliyompa ni ile ambayo ukifa ukiwa umeivaa basi unaenda peponi moja kwa moja. Akaichukua na kuiweka kwenye mkoba. Wakati tunaunganisha ndege kutoka Uingereza kwenda Jamaica, katikati ya safari, mvua kubwa na radi na upepo mkali ukaanza kupiga, na ndege yetu ikaanza kupata msukomsuko(turbulence) mkubwa sana. Hakika nilikuwa sijawahi kuona msukosuko mkubwa kama huo. 
Siti yangu ilikuwa karibu na bawa, na nikichungulia nje ya bawa naona wakati wowote linaweza kukatika. Kulikuwa maombi na vilio vya kila aina. Hii ndiyo siku ambayo nilikuwa na hakika ingekuwa mwisho wa uhai wangu. Nikaomba dua zote. Nikatoa shahada (ash-haddu...) mara kadhaa. Sasa nikimuangalia jamaa yangu pembeni yangu niliyempa ile rozari naona katulia tu. Nikakumbuka maneno yake kwamba ukifa ukiwa umeivaa ile rozari basi unaenda peponi moja kwa moja. 

Nikamwambia “eh bwana hebu niazime ile kitu mara moja”. Nikiwa nawaza huwezi kujua labda maneno yake yalikuwa na ukweli. Sio kwa upungufu wa imani yangu, bali kuwa na mlango wa ziada kama huyu bwana alikuwa sahihi. Kumbe kishaitoa kwenye mkoba na boksi lake kishaivaa zamani, kimya kimya. Nikaendelea na dua zangu. Wingu likapita. Imani yangu ikaimarika.

Image result for animated download now gif

No comments

Powered by Blogger.