HESLB YAANZA KUPOKEA MAOMBI YA MIKOPO
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa muda wa miezi miwili na kusisitiza kuwa maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao..
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema leo jijini Dar es salaam wakatik akifungua rasmi kuwa mtandao wa kuwasilisha maombi ya mkopo (www.olas.heslb.go.tz) utakuwa wazi kuanzia Mei 10, 2018 hadi Julai 15, 2018 ili kuwapa fursa wanafunzi wahitaji kuwasilisha maombi yao.
“Mwaka jana tulitoa mwezi mmoja, mwaka huu tumetoa muda zaidi ili kuwawezesha kusoma mwongozo kwa makini na kuzingatia maelekezo tunayoyatoa,” amesema Bw. Badru katika mkutano na wanahabari ambapo pia alizungumzia mambo muhimu yaliyomo kwenye mwongozo unaojumuisha sifa na taratibu za utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019. Mwongozo huo unapatikana katika lugha za Kiswahili na Kiingereza kwenye tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz)
Mambo muhimu yaliyomo kwenye Mwongozo
Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa katika utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019, kipaumbele kitatolewa kwa watanzania wahitaji wanaosoma kozi zenye uhitaji mkubwa zaidi kitaifa kama walimu wa masomo ya sayansi na hisabati; na sayansi ya afya ya binadamu.
“Tutatoa kipaumbele pia kwa waombaji mikopo watakaodahiliwa katika kozi zinazohitajika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kama uhandisi wa aina zote; kozi za sayansi za kilimo na wanyama na kozi zinazohusiana na gesi na nishati,” amesema Bw. Badru katika mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa wadau wa HESLB kama Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO); Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Shirika la Posta (TPC).
Aidha, ameongeza kuwa watanzania wahitaji ambao ni yatima na wana nakala za vyeti vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) nao watapewa kipaumbele bila kujali kozi wanazosoma. Wengine watakaopewa kipaumbele ni waombaji wenye ulemavu uliothibitishwa na Mganga wa Mkoa au Wilaya na waombaji mikopo ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya stashahada (diploma) au sekondari na wana barua za uthibitisho kutoka taasisi zilizowafadhili.
Bajeti na idadi ya watakaopata mikopo kwa 2018/2019
Kuhusu malengo ya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019, Bw. Badru amesema Bodi imepanga kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi wapya 40,000 na wanaoendelea zaidi ya 80,000. Kati yao, wanawake watakuwa asilimia 35 (14,000) na wanaume asilimia 65 (26,000). Bajeti ya fedha za mikopo kwa mwaka 2018/2019 ni TZs 427 bilioni.
Maboresho yanayoendelea
Kuhusu uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, Bw. Badru amesema Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Kitengo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UCC) wanaendelea na maboresho makubwa ili kuifanya mifumo ya utoaji na urejeshaji mikopo kuwa rafiki zaidi kwa wateja. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.
“Kwa mfano, mfumo wa kuwasilisha maombi sasa umeboreshwa na kuwa rafiki zaidi kwa kuwa unamwongoza mwombaji katika kila hatua – na hatoweza kwenda hatua inayofuata kabla ya kukamilisha hatua ya awali,” amesema Bw. Badru.
Aidha, kwa mara ya kwanza, Bodi imetoa mwongozo wake wa uombaji mikopo katika lugha ya Kiswahili pamoja na kitabu chenye maswali na majibu 21 kuhusu sifa na utaratibu (hatua kwa hatua) wa kuwasilisha maombi ya mikopo. Kitabu na mwongozo vinapatikana katika tovuti ya Bodi na vitasambazwa kwa wadau kuanzia wiki ijayo ambapo maafisa wa Bodi watatembelea shule na waombaji nchini kote.
Maoni ya TAHLISO
Akiongea katika mkutano huo, Meneja Usajili wa RITA Bi. Patricia Mpuya amewahakikishia waombaji wa mikopo kuwa vyeti vya vifo na kuzaliwa ambavyo vitawasilishwa kwa taasisi hiyo kuwa vitahakikiwa ndani ya siku tatu.
“Tunawakumbusha kuhakikisha wanaleta maombi haraka badala ya kusubiri ‘deadline’ (muda wa mwisho) na sisi tumejipanga wanapata majibu ya uhakiki ndani ya siku tatu tangu tuyapokee,” amesema Bi. Mpuya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shirika Posta (TPC) Bw. Hassan Mwangombe, ambao watapokea na kusafirisha kwenda HESLB fomu za maombi ya mikopo, amesema wamejipanga kutoa huduma za elimu kwa waombaji na intaneti katika vituo vyao zaidi ya 180 nchini. Aidha, wameandaa bahasha maalum ambayo mwombaji mkopo atajaza taarifa zake muhimu ili kurahisisha uwasilishaji wa maombi hayo kwa HESLB.
Mwenyekiti wa TAHLISO Bw. George Mnali amezitaka RITA na TPC kuhakikisha wanatekeleza mipango yao ya kuwahudumia waombaji mikopo kama walivyoahidi na kuongeza TAHLISO itatumia muda wa miezi miwili kuwaelimisha wanafunzi wasio na mikopo lakini wana sifa kuomba na kufuata maelekezo ya Bodi.
Wito
Bodi imewataka waombaji mikopo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wale ambao wana uwezo wa kugharamia elimu ya juu kutoomba mkopo ili kutoa fursa kwa wahitaji halisi wengi zaidi kuomba na kupata mikopo.
HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na wenye sifa na kukusanya mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.
Imetolewa na:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Leave a Comment