MATUKIO YALIYOTOKEA KIPINDI JAMIIFORUMS HAIPO HEWANI
Juni 10, 2018. Riverside, DAR: Wanafunzi wa UDSM wafariki katika ajali ya gari la Wagonjwa na Lori
Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Dar Es Salaam(DARUSO) ilitoa taarifa ya ajali ambapo wanafunzi wawili Maria Godian Soko(Mwaka wa kwanza COSS) na Steven E Sango(CPE CoET mwaka wa pili) na dereva James Josephat walifariki Dunia.
Mwanafunzi mwingine aliyekuwepo katika msafara huo Abishai Nkiko(Bsc Industrial Engineering mwaka wa 3 CoET) alikuwa katika hali mbaya na kukimbizwa katika hospitali ya Muhimbili. Huku Mfanyakazi mwingine wa chuo hicho, Jonadhan Lugendo ambaye naye alipata majeraha alifariki akiwa hospitalini Muhimbili. Maria Godian Soko alikuwa anakimbizwa hospitali baada ya kubanwa na pumu hali iliyomfanya kupoteza fahamu.
Juni 13, 2018, DAR: Wakurugenzi sita kutoka Bodi ya Mikopo HESLB watumbuliwa
Wakurugenzi sita wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wameachishwa kazi kwa makosa mbalimbali ikiwamo uzembe na kuisababishia serikali hasara ya Tsh. Bilioni 21.3
Wakurugenzi hao ni Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Juma Chagonja, Mkurugenzi wa Upangaji na Ugawaji Mikopo, Onesmus Laizer na Mkurugenzi Msaidizi wa Ugawaji Mikopo, John Elias. Wengine ni Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo, Robert Kibona, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, Heri Sago na Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo, Chikira Jahari
Juni 14, 2018, Mbeya: Ajali yaua Wanajeshi wa JWTZ na JKT
Gari lililokuwa limebeba Askari wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) lilianguka na kusababisha vifo vya wanajeshi 12 wa JKT na mmoja wa JWTZ pamoja na majeruhi Jijini Mbeya
Chanzo cha ajali hiyo kimesekana kuwa ni mwendokasi uliopelekea gari kukatika kwa ‘break’ kutokana na mteremko mkali katika eneo la Igodima na kuangukia korongoni.
Juni 14, 2018, Dodoma: Serikali yawasilisha Bungeni Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2018/19
Serikali imewasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha inayotarajiwa kuwa Tsh. Trilioni 32.48, huku akibainisha maeneo saba yaliyopewa msukumo
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliyataja maeneo hayo ya kipaumbele kuwa ni kilimo, viwanda, elimu, miundombinu, afya, upatikanaji wa maji na urasimishaji ardhi. Maeneo mengine ya kipaumbele ni kurahisisha umiliki wa ardhi, kuimarisha huduma za mawasiliano, kifedha na utalii na kuimarisha ulinzi, usalama, utawala bora na utoaji haki.
Juni 16, 2018, Dodoma: Serikali yatangaza waliochaguliwa kujiunga Kidato cha tano na chuo cha ufundi
Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano 2018 na vyuo vya ufundi 70,904 kati ya 95,337 waliofaulu
Wanafunzi 24,433 ambao walikuwa na sifa za kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2018, wamekosa nafasi kutokana na ufaulu kuongezeka ikilinganishwa na nafasi zilizopo
Juni 18, 2018, Dodoma: Wabunge wa Upinzani watoka Bungeni baada ya Bajeti mbadala kuzuiwa kusomwa Bungeni
Baada ya bajeti hiyo uzuiwa kusomwa Wabunge wa upinzani (isipokuwa wanaomuunga mkono Prof Lipumba) walitoka kwenye ukumbi wa Bunge baada ya bajeti mbadala kuzuiwa kusomwa bungeni.
Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa upande wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde amesema aliwasilisha mapendekezo ya bajeti mbadala kwa Katibu wa Bunge jana Juni 17, 2018 saa nane mchana lakini ofisi yake ikazuia kuchapishwa na ofisi ya Bunge.
Silinde amesema Kanuni ya 99(5) ya Bunge imevunjwa kwani upinzani waliwasilisha taarifa yao bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango lakini imeondolewa bila sababu kutolewa. Vipaumbele vya bajeti mbadala kwa mwaka 2018/19 ni Elimu, Mapinduzi ya Kilimo, Viwanda katika mnyonyoro wa kilimo, huduma za afya kwa wananchi na upatikanaji wa maji.
Juni 19, 2018, Dodoma: Serikali yakamata samaki wasiostahili kuvuliwa katika Mgahawa wa Bunge
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilikamata samaki wasiostahili kuvuliwa wakiwa tayari kwa matumizi kwenye Mgahawa wa Bunge na kumpiga mmiliki wa Mgahawa huo Daniel Lamba, faini ya Tsh. 300,000 baada ya kukiri kosa la kukutwa na kilo 3 za samaki hao aina ya sato
Spika wa Bunge, Job Ndugai alieleza masikitiko yake kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kitendo cha maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuingia kwenye mgahawa uliopo bungeni pasipo taarifa na kuanza kupima samaki akisema kilichofanyika ni dharau. Ndugai alitoa kauli hiyo baada ya kutangaza kumsamehe Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ambaye aliwasilisha maelezo ya Serikali kuhusu tukio hilo, huku wabunge wakimtaka waziri huyo kujitathimini
Juni 19, 2018: Shirika la Ndege la Etihad lasitisha safari zake za Abu Dhabi na Dar es Salaam
Shirika la Ndege la Etihad limetangaza kusitisha safari zake kati ya Abu Dhabi na Dar es Salaam kuanzia Jumatatu Oktoba 1, 2018. Etihad Airways ilitangaza kupata hasara ya $ bilioni 1.87 toka Juni 2017
Juni 20, 2018, Kisutu-Dar: Vigogo wa Halotel na Zantel wahukumiwa Kifungo cha miaka 7 au faini, walipa faini wakwepa jela
Vigogo wa kampuni za Zantel na Halotel walikwepa kifungo cha miaka 7 jela baada ya kufanikiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 238.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kuwaamuru wakurugenzi watendaji wa kampuni hizo, wanaokabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kulipa fedha hizo pamoja na hasara waliyoisababisha ya Tsh. Bilioni 1.1. Vigogo hao ni mkurugenzi wa Halotel raia wa Vietnam, Le Van Dai (35); Mkurugenzi mkuu wa Zantel raia wa Misri, Sherif El Barary; Msimamizi wa biashara wa Halotel Zanzibar, Jimmy Mosha (26); Meneja Masoko Halotel, Willy Ndoni (29)
Juni 24, 2018, Sumabwanga: Baraza la Maaskofu wa Katoliki(TEC) latangaza uongozi wake Mpya
Uongozi wa TEC ulitanganzwa na Mhashamu Taricisius Ngalalekumtwa:
Rais wa TEC, Gervas Nyaisonga - Askofu wa Mpanda.
Makamu Rais wa TEC, Flavian Kasala - Askofu wa Geita.
Katibu wa TEC, Padre Charles Kitima - Jimbo la Singida
Aidha, Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Fransisko, amemteua Mhashamu Askofu Mkuu Jude Thaddeus Ruwa’ichi, kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Juni 25, 2018 Mkuraga, Pwani: Ajali ya Daladala na Lori yaua watu 14 wa familia moja
Watu 14 wa familia moja waliokuwa wakielekea katika mahafali ya JKT Msata wamefariki na wengine 4 kujeruhiwa baada ya Gari dogo kugongana uso kwa uso na Lori la mchanga lenye namba za usajili T 439 DCC.
Kamanda wa Polisi Rufiji, Onesmo Lyanga amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 10 alfajiri, huku chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Lori alikuwa amesinzia.
Juni 25, 2018, Bungeni Dodoma: Nape Nnauye na Hawa Ghasia wazungumzia ushuru wa 65% unaotokana na mauzo ya Korosho
Wabunge wa CCM, Nape Nnauye(Mtama) na Hawa Ghasia(Mtwara Vijijini) wamesema hawakubaliani na mapendekezo ya Serikali ya kufuta ushuru wa asilimia 65 wa fedha zinazotokana na mauzo ya korosho nje na kubainisha kuwa kinachofanywa ni kuiua CCM mikoa ya Kusini.
Katika mjadala wa bajeti ya Serikali, wamesema wapo tayari kudhalilishwa na wabunge wenzao waliopangwa kuitetea Serikali katika suala hilo la Korosho huku mawaziri wawili wakisimama kutetea jambo hilo.
Tayari baadhi ya wabunge wametishia kufanya maandamano iwapo Serikali haitatoa asilimia 65 za ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo. Pia, wanapinga mabadiliko ya Sheria ya Korosho yanayokusudiwa kufanywa na Serikali ili ushuru huo upelekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.
Juni 26, 2018, Dodoma: Bunge lapitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19
Bunge laidhinisha Tsh. Trilioni 32.476 kwa ajili ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha
Bajeti hiyo lilipitishwa kwa jumla ya kura 266 za ndiyo, huku kura 82 tu zikiwa zimesema hapana. Wabunge 43 hawajapiga kura kutokana na kutokuwepo ndani ya bunge.
Juni 30, 2018, Dodoma: Fedha kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbubukumbu za Mashujaa kutumia kujenga Barabara
Agizo hilo limetolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuagiza kuwa Tsh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
Ametaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari katika barabara ya Kisasa na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya Emmaus-African Dream yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha lami. Kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka Tanzania huadhimisha siku ya mashujaa.
Leave a Comment