WAZIRI KANGI LUGOLA ATAKA DHAMANA ZITOLEWE HADI SIKU YA JUMAPILI


Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amekemea utaratibu wa watuhumiwa kunyimwa dhamana hasa siku za mapumziko kwa kisingizio kuwa si siku za kazi. Akizungumza leo Jumapili Septemba 30, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Busanza wilayani Uvinza mkoani Kigoma, Lugola amesema dhamana kwa mtuhumiwa inapaswa kutolewa saa 24 na siku zote za wiki. Amesema vituo vya polisi nchini vinafanya kazi siku zote za wiki zikiwemo za mapumziko, kuahidi kutomfumbia macho askari yeyote atakayeshindwa kutoa dhamana kwa kosa ambalo lina dhamana..


“Hii tabia sijui imetoka wapi na imejengeka kwa baadhi ya askari polisi. Eti mtu akiingia mahabusu siku ya Ijumaa ikifika Jumamosi na Jumapili hawatoi dhamana wakisema mpaka Jumatatu, hii tabia sio sahihi na ife haraka iwezekanavyo,” amesema Lugola. Amesema dhamana ni haki ya mtu endapo kosa lake linadhaminika huku akiwataka wananchi watakaoombwa fedha ili wapewe dhamana kuripoti tukio hilo kwa maofisa wa ngazi za juu ili askari husika achukuliwe hatua za kinidhamu. “Kuna tabia iliyozoeleka katika jamii, eti kuingia polisi ni bure ila kutoka ni fedha, hii kauli nataka ife kwasababu nawajua polisi na hawanidanganyi kwa lolote,” amesema.

Chanzo: Mwananchi

Image result for animated download now gif

No comments

Powered by Blogger.