DARAJA LA AJABU LINALOONGOZA KWA MBWA 'KUJINYONGA'


Daraja la Overtoun lililopo Dumbarton nchini Scotland, limeweka rekodi ya ajabu kwa maelfu ya mbwa kujirusha mpaka chini, umbali wa mita 50 na kudondokea kwenye mawe na kufa papo hapo.


Awali lilionekana kama ni jambo la kawaida lakini kadiri watu wengi zaidi walivyokuwa wakilalamikia mbwa wao kujirusha na kufa kwenye daraja hilo, liligeuka na kuwa gumzo kubwa, kila mtu akizungumza lake, wengine wakilihusisha na mambo ya kishirikina kwamba kuna mzimu hatari unaopendelea damu ya mbwa unaoishi chini ya daraja hilo. Daraja la Overtoun au maarufu kama ‘Dog Suicide Bridge’ lilijengwa mwaka 1895 na mkandarasi wa Kiskochi, Henry Ernest Milner likiwa na urefu wa mita 15 kwenda chini, likiunganisha eneo maarufu la mashambani la Overtoun.

Matukio ya mbwa kujirusha yalianza kuripotiwa kwa wingi kwenye miaka ya 1950 na 1960 na yameendelea kuwepo hadi leo, huku pia kukiripotiwa matukio mengine ya watu kujiua au maiti za watu kuokotwa chini ya daraja hilo ingawa idadi yake ni ndogo ukilinganisha na mizoga ya mbwa wanaojirusha kutoka juu ya daraja hilo. Hali hiyo ilisababisha mamlaka zinazohusika kuweka vibao vya tahadhari kwenye pande zote mbili za daraja hilo, kuwatahadharisha watu wanaopita na mbwa wao kwenye eneo hilo, kuhakikisha kwamba wamewafunga vizuri kamba au minyororo shingoni na kuwashika kwa nguvu ili kuepuka kujirusha mpaka chini na kufa.

Si hivyo tu, watafiti mbalimbali wa tabia na hulka za wanyama, kwa kipindi kirefu nao waliendelea kuchunguza kinachosababisha matukio hayo. Na kilichosumbua zaidi vichwa vya wengi, ni kwamba matukio yote ya mbwa kujirusha, yalikuwa yakitokea upande mmoja wa daraja na hakuna hata moja lililotokea upande wa pili. Mtaalamu wa saikolojia ya wanyama, Dr. David Sands baada ya kufanya utafiti kwa muda mrefu alikuja na majibu ya kitaalamu. Alisema chini ya daraja hilo kuna wanyama wadogo jamii ya vicheche (minks) ambao kwa kawaida hupenda kuishi kwenye mashimo na mapango kandokando ya mto. Akaongeza kwamba wanyama hao hukojoa mkojo ambao harufu yake huwavutia sana mbwa ambao pia hupenda sana kuwala wanyama hao, kwa hiyo mbwa wakipita eneo hilo na kusikia harufu hiyo, tena ikitokea chini ya daraja hujikuta wakiruka kwa lengo la kuwafuata wanyama hao.



Hata hivyo, utafiti huo ulipingwa vikali na John Joyce, mwindaji na mkazi wa eneo hilo aliyefanya kazi ya uwindaji eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50 ambaye alisema hakuna wanyama hao eneo hilo. “Hakuna kabisa, hakuna wanyama hao kwenye eneo hili, nimewinda kwa miaka chungu nzima lakini sijawahi kuwaona, ni uongo,” alinukuliwa John. Sababu iliyoonekana kukubalika na wengi ni kwamba kuna ‘zimwi’ chini ya daraja hilo, ingawa hakuna aliyeweza kulithibitisha hilo kisayansi..!
Image result for animated download now gif

No comments

Powered by Blogger.