WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDATO CHA NNE 2018 NA KUFAULU WAPANGIWA SHULE ZA ELIMU YA JUU NA VYUO VYA UFUNDI

Jumla ya wanafunzi 108,644 sawa na asilimia 98.31 ya wanafunzi wote wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na kidato cha Tano,Vyuo vya Elimu ya Ufundi na vyuo vingine vinavyosimamiwa na Baraza la Elimu ya Ufundi.

Aidha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano pekee ni 69,356 sawa na asilimia 62.76 ya wanafunzi 110,505 waliokuwa na sifa,ambapo wasichana ni 31,809 na wavulana ni 37,547.

Akitoa taarifa kuhusu uchaguzi huo kwa Mwaka 2019,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mh.Seleman Jafo amesema kuwa kati ya wanafunzi hao wasichana wote wamepata nafasi na wavulana 1,861 wamekosa nafasi ambapo watapatiwa nafasi katika chaguo la pili.

Waziri Jafo ameongeza kuwa Muhula wa Kwanza wa masomo kwa wanafunzi wa kidato cha tano utaanza July 08 mwaka huu,hivyo wanafunzi wote waliochaguliwa wanapaswa kuripoti ndani ya siku 14 kuanzia tarehe hiyo na kuwa endapo mwanafunzi atashindwa kuripoti ndani ya siku hizo nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

Kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi vilivyo chini ya Baraza la Elimu la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wao wametakiwa kuthibitisha kujiunga na kozi zinazosimamiwa na Baraza hilo kuanzia June 09 mwaka huu. Hata hivyo,Orodha ya wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi inapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz 

No comments

Powered by Blogger.