MAMBO 20 AMBAYO HUTAKIWI KUMWAMBIA MTOTO WAKO
Mara kadhaa wazazi wamekuwa wakiwaambia watoto wao maneno mbalimbali wakati wakiwa na furaha au hasira. Ipo nguvu kubwa kwenye maneno ya kutamkiwa ambayo wazazi wengi hawaifahamu.
Kwa hakika maneno yanaweza kujenga au kubomoa maisha ya mtoto kwa kiasi kikubwa. Hivyo fahamu maneno 20 ambayo hutakiwi kumwambia mtoto wako.
1. Wewe ni mtoto mbaya
Wazazi wengi wanapokasirishwa na mtoto humwambia wewe ni mtoto mbaya, hili humfanya mtoto ajione hafai.
Hivyo ni vyema kuepuka kumwambia mtoto neno hili badala yake mweleze kosa lake na athari zake ili aliepuke.
2. Kwanini usiwe kama dada au kaka yako?
Kauli hii humfanya mtoto ajione dhaifu kwa sababu unamlinganisha na wengine. Kauli hii pia humjengea chuki na wivu kwa wale unaowataja kwake kuwa ni bora. Hili husababisha watoto kuchukiana kwa kuwa mzazi anapenda baadhi yao au mmoja wao.
3. Huwezi hili
Mwache mtoto ajaribu ashindwe na si wewe kumwambia kuwa hawezi. Wewe kama mzazi unapaswa kuwa hamasa kwa mtoto na si kumkatisha tamaa.
4. Usiongee na mimi
Kama hautaki mtoto wako aongee na wewe, je unataka aongee na nani? Ukiwa umekwazwa na mambo yako, usihamishie matatizo hayo kwa mtoto.
Kumbuka mtoto naye ana haki ya kusikilizwa, msikilize na umjibu kama inavyotakiwa.
5. Wasichana au Wavulana hawafanyi hivyo
Kumwambia mtoto neno hili ni kumwonyesha kuwa kuna jinsia fulani bora au yenye nguvu zaidi. Hivyo ni vyema kutokumwambia mtoto neno hili, mwache akue na atatambua mwenyewe kama kuna jinsia dhaifu au yenye nguvu zaidi.
6. Niache
Wazazi wengi hupenda kuwaambia watoto wao “niache” “nina kazi niache” “usinisumbue”, n.k. Kumbuka kuwa wewe ni kila kitu kwa mtoto wako, je unataka akuache aende kwa nani?
Tenga muda na uwe karibu na mtoto wako ili umuhudumie na kumsaidia kwa njia mbalimbali.
7. Hakuna mtu anamtaka mtoto kama wewe
Kuna wazazi huwajengea watoto roho ya kukataliwa tangu wakiwa wadogo sana. Kumwambia mtoto maneno haya humfanya ajione duni na mwenye kukataliwa; hivyo epuka maneno haya.
8. Umeshakuwa usifanye hivi
Jumkumu lako siyo kumhamisha mtoto hatua moja ya ukuaji kwenda hatua nyingine bali ni kumlea sawa sawa na maadili.
Kama mtoto anamalizia utoto wake mwache amalizie asije akacheza ukubwani. Mwache afurahie na kuutumia utoto wake vyema kwani kuna kipindi atacha utoto yeye mwenyewe.
9. Wewe ni mvivu
Mtoto akishatambua kuwa wewe unamwona ni mvivu, kamwe hawezi kuwa na bidii ya kazi. Mtoto anaposhindwa kufanya kazi vyema, mhamasishe na kumtia moyo badala ya kumwambia wewe ni mvivu.
10. Unaninyima raha wewe mtoto
Mara nyingi watoto wanapowakwaza wazazi, wazazi huwaambia kuwa wanawanyima raha. Je kama unamwambia mtoto kuwa yeye siyo chanzo cha furaha kwako ni nani atakayekupa furaha?
Mtoto akijua kuwa yeye hakupi furaha, wala yeye hatokuona kuwa wewe unampa furaha.
11. Unaishi kwenye nyumba yangu ni lazima ufuate sheria zangu
Hili ni swala ambalo linafanywa na wazazi wengi sana; wao huwafanya watoto kama wapangaji au wageni na si sehemu ya familia.
Kumwambia mtoto kuwa hapa ni kwangu humfanya ahisi kuwa yupo mahali ambapo si kwake na hastahili kuwa hapo. Mjeengee mtoto hisia za umiliki (sense of ownership) huku ukimuelekeza kuwa na maadili mema.
12. Kila kitu changu ni chako
Inawezekana una mali nyingi ambazo kweli kabisa ni za mtoto wako, lakini unapaswa kumjengea mtoto akili ya kutafuta na si kumpumbaza kwa mali ulizo nazo.
Kumwambia mtoto kila kitu changu ni chako, humfanya asifanye bidii au aone ana haki ya kupata na kutumia kila kitu jinsi apendavyo.
13. Nakupenda kuliko watoto wangu wote
Kauli hii humfanya mtoto awe mbaguzi na aone kuwa kuna ubaguzi na upendeleo kwenye familia. Hata kama unampenda mtoto fulani zaidi, basi usimwambie mtoto mwingine.
14. Siwezi kukukatalia kitu
Je akija akitaka roho yako utampa? Kauli hii ni mbaya humfanya mtoto akutawale na aone kuwa unatakiwa kutii, kukubali na kumpa kila anachokitaka.
15. Usiongee na watu usiowajua au fulani
Kama una chuki zako, zimalize wewe mwenyewe na si kuzihamishia kwa mtoto. Mtoto anapokuja duniani hutafuta kujenga mahusiano na watu na si kujenga chuki na matengano.
16. Sitakusamehe
Mzazi anapaswa kuwa mfano mzuri wa kumfundisha mtoto kusamehe. Ikiwa wewe humsamehi anapokukosea, je unafikiri atakuwa na roho ya kusamehe wengine? Mfundishe mtoto kusamehe.
17. Ngoja baba yako aje
Hii ni kauli inayopendwa sana na wazazi wengi hasa wakina mama.
Kauli hii humfanya mtoto amwogope baba na amwone kama adui, pia humfanya mtoto amwone mama kuwa ni dhaifu, ikiwa baba hayupo mtoto atafanya makosa kwani anajua mama hamfanyi kitu.
18. Matusi yote kwa ujumla wake
Mtoto mtukanaji mara nyingi anaishi kwenye familia inayotukana. Utamkuta mama anamwita mtoto mbuzi, ng’ombe, shetani, jambazi, paka, nguruwe, mbwa n.k. je kweli ulizaa vitu hivi na si binadamu?
Unapomtukana mtoto, naye hujifunza kuwatukana watu wengine. Pia humwathiri kisaikolojia na kiroho na kumfanya awe kama kile unachomwita.
19. Nitakumaliza au nitakuua
Baadi ya wazazi huenda mbali zaidi na kuwaambia watoto wao maneno ya kuwatishia kuwadhuru vibaya au kuwaua.
Hili humwathiri mtoto kisaikolojia na kumjengea tabia ya kuwatishia au kuwadhuru watu wengine. Kama mtoto anatishiwa kuuwawa na wewe ni nani atakayemlinda?
20. Acha kulia haraka au usilie
Kulia ni njia moja wapo ya mtoto kueleza hisia zake. Kumzuia mtoto kulia ni sawa na kumkataza kuweka wazi hisia zake. Mwache alie kama hana maradhi, kwani baada ya muda atachoka na kunyamaza mwenyewe.
Neno la mwisho
Kwa hakika kauli au maneno mengi mabaya huwatoka wazazi mara wanapokuwa na hasira au wanapokwazwa na watoto wao. Ni vyema kutawala hisia zako na kuhakikisha unamfahamisha mtoto kosa lake, madhara ya kosa hilo na jinsi ya kuliepuka.
Je wewe ulishamwambia mtoto wako maneno haya au kuyasikia kwa mtu mwingine? Tafadhali toa maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.
Leave a Comment