JINSI YA KUJIUNGA NA FREEMASONS
Ifahamike kwamba, kujiunga na Freemasonry imekuwa ni ishu tata kwa sababu ni mtandao tata ambao uko kinyume na masuala ya Mungu wa kweli lakini katika simulizi hii, kitendo cha kueleza jinsi ya kujiunga na Freemasonry, kusudi kubwa ni kuangalia namna watu wanavyojiunga na siyo kushawishi mtu yeyote kujiunga...
Mwanachama mpya hushauriwa kutafuta Jumba la Freemasons linaloitwa Masonic Lodge lililopo karibu naye na kuwasiliana nao na kueleza nia yako ya kujiunga nao baada ya kujiridhisha kuwa una habari kamili zinazowahusu. Usiwe mdandiaji wa masuala usiyoyajua undani wake. Ni vizuri ukatafuta habari kamili inayohusu kitu unachokitaka.
Mtu anayetaka kujiunga na jamaa hao hutiwa moyo kuwa unapokuwa umejiunga, utakuwa umejiunga na familia kubwa na ya zamani sana ya watu wenye nia zinazofanana duniani (the oldest and largest fraternity in the world). Makabrasha yao yanaonesha kwamba, ukibahatika kujiunga nao, utakuwa umejiunga na ndugu zaidi ya 2,000,000 kutoka kila jamii na rangi na dini na taifa na kila kitembeacho duniani kutafuta maisha au uhai. Kujiunga na Freemasonry ni hiyari yako na kujitoa pia ni hiari yako. Wenyewe wanadai ni uhusiano wa kidugu unaounganisha wanaume wenye mapenzi mema na tabia njema na maadili na wanaotetea haki kila mahali duniani, wanaomwamini Mungu mwenyezi, muumba wa mbingu na ardhi na wanaopenda kuendeleza roho ya umoja na udugu kwa wanadamu.
Jumuiya hiyo inahitaji watu watiifu kwa taifa lao na wanaojitoa wakati wote katika kanuni za urafiki na umoja na ushirikiano. Lengo lao kuu ni kuihudumia jamii inayowazunguka. Kwa wanaume wengi, Freemasonry huwa inatimiza sehemu ya ndoto zao zinazoonekana kutoweka, kwa namna iwayo yote katika jamii, falsafa, kiroho, kihistoria na kadhalika. Kwa ufupi masuala yote yahusuyo jamii utakutana na Freemasons na kutimiza sehemu ya kile unachokitafuta. Kama kweli ukitaka kujiunga na Freemasons lazima kujua ni nini hasa malengo yao na yako? Freemasons wana mpango wa kujenga dunia iliyo bora ‘better world’ katika njia ya kipekee na inayostahili na kuandaa wanaume wema kuishi katika ulimwengu huo. Usemi mkuu wa Freemasons wa sasa ni ‘wanaume wema hufanya dunia njema’.
Ukiwa Freemason utajifunza kutendea kazi, suala la kuwapenda watu kwa njia zote, ukarimu kwa watu wenye uhitaji, maadili na kuwa raia mwema katika kila jamii. Freemasons ni wajenzi wenye ukarimu, upendo, elimu na wenye kujenga maadili. Suala kuu zaidi ni kuwa watendaji katika suala la udugu wa wanaume chini ya ubaba wa Mungu. Pia Freemasons wanalenga kutoa elimu katika nyanja mbalimbali na kukufanya uwe mtaalam mzamivu, yaani master katika shahada za Freemasonry. Kwa msingi huo, Freemasons wanatia moyo na kusaidia jamii kupata elimu na pia wanafundisha wanachama wao maadili na udugu kwa kutumia njia za sherehe na ishara au alama.
Usisahau, wenyewe wanajinasibu kuwa wanatoa fursa ya udugu na nafasi sahihi na kuchochea au kutia moyo wanaume kukusanyika katika makundi na kufurahi na kuendeleza utu. Kwa mujibu wao, Freemasons wanapaswa kuwa watu wa kuwajibika na kuwa na bidii katika mkazo wa uthamani wa utu na utakatifu na kutimiza wajibu. Kila Freemason mwenye digrii ya tatu, hupandishwa daraja na kuwa master. Kila mwanachama anapaswa kuwa na bidii kuiendeleza jamii katika masuala yote yanayohusu ustawi wa mwanadamu, kuhamasisha jamii kuwa na hisia za ukarimu na mapenzi mema kwa wanadamu wote ikiwa ni pamoja na kutafasiri kanuni tunazojifunza na kuwa na ushawishi kivitendo.
Leave a Comment