UMUHIMU WA MAJI KWENYE MWILI WA BINADAMU
Kunywa maji safi na salama kwa kiasi kinachostahili kiafya kunaweza kuyaboresha maisha yako na kukufanya ujihisi mwenye afya na furaha zaidi. Kunywa maji ya kutosha kuna faida nyingi. Tukichukulia kunywa maji ya kutosha ni mithili biashara kati ya wewe na afya yako, biashara hii inalipa.
Zifuatazo ni baadhi ya faida za kunywa maji ya kutosha.
Vimengenya na Kemikali mbalimbali zinazohusika na mmen'genyo au usagaji wa chakula mwilini ziko katika hali ya mchanganyiko na maji. Ili hivi viweze kufanya kazi vizuri inatakiwa kuwe na uwiano sahihi kati yake na maji.Pia maji yanahusika katika kulainisha baadhi ya vyakula .
Pia kunywa maji ya kutosha kunaongeza ufanisi wa mwili katika kusharabu chakula.
Mara nyingine maumivu ya kichwa yanasababishwa na upungufu wa maji mwilini. Hii inamaanisha, kama una maumivu ya kichwa yanayosababishwa na upungufu wa maji mwilini unaweza kughairi kumeza vidonge vya kutuliza maumivu na kunywa maji. Hii inawezekana kwenye baadhi ya maumivu ya mgongo pia.
Pendezesha ngozi yako kwa kunywa maji ya kutosha.
Unaweza kuboresha sura na mguso wa ngozi yako kwa kunywa maji ya kutosha kwani maji yanasaidia kuboresha tishu za ngozi na kuongeza unyevu kwenye ngozi .
Maji yanauweka ubongo katika hali nzuri zaidi na ya ufanisi zaidi. Kunywa maji ya kutosha kunamwezesha mtu kufikiria kwa ufanisi zaidi.
Sehemu kikubwa ya haja kubwa ni maji. Kunywa maji ya kutosha kunaweza kukusaidia kupata haja kubwa kiulaini na mara kwa nyingi zaidi.
Maji ya kutosha yanasaidia kupunguza tatizo la kubanwa misuli na pia hupunguza msuguano katika viungo vyako.
Maji yanachochea shughuli za kimetaboliki mwilini na kuongeza ufanisi wa ubongo kwa hiyo yanapunguza uchovu.
Uwezekano wa kupata mafua,mawe ya figo,matatizo ya ini,baadhi ya saratani n.k unaweza kupunguzwa kwa kunywa maji ya kutosha.
Kama uko katika mkakati wa kupunguza uzito maji yanaweza kukusaidia kwa kiasi kikubwa. Maji huongeza kasi ya shughuli za kimetaboliki mwilini. Ongezeko hilo la kimetaboliki husababisha mwili kutumia nishati nyingi zaidi na hivyo huweza kupunguza kiasi cha nishati ambacho kitahifadhiwa mwilini katika hali ya mafuta au kupunguza kiasi cha nishati kilichohifadhiwa mwilini. Pia ongezeko la ufanisi wa figo na ini kutokana na kunywa maji ya kutosha husaidia kutoa mazao ya mafuta ya ziada mwilini.
Maji hayaongezi nishati mwilini, kwa hiyo unywapo maji badala ya juisi,soda au vyakula au vinywaji vingine ambavyo huongeza nishati au mafuta mwilini unaongeza uwezekano wa kupungua uzito.
kunywa maji ya kutosha kutakufanya ujisikie vizuri na pia kunaweza kupunguza safari za hospitali. Kunywa maji ya kutosha, fanya siku yako iwe poa zaidi.
Leave a Comment