MAJAMBAZI WA KENYA WALIVYOTIKISA NA KUWEKA HISTORIA NCHINI TANZANIA - 2

SEHEMU YA PILI

Wazo kupitishwa ndo mwanzo wa kurudi tena swali gumu lile la mwenyeji wao atakuwa nani nchini TANZANIA maana jamaa waliyemzoea na kufanya naye biashara za kihalifu nchini TANZANIA hakuwa duniani tena baada ya kuuliwa na polisi jijini ARUSHA.

Jambazi huyu alikuwa akijulikana kama FRANK LYATUU mkazi wa NGARAMTONI na mmoja wa majambazi sugu walioshindikana jijini ARUSHA na mhusika wa tukio kubwa la ujambazi jijini DAR ES SALAAM lililofanyika UBUNGO MATAA na kujulikana kama UWIZI MKUBWA UBUNGO MATAA.

UWIZI MKUBWA UBUNGO MATAA ni ule uwizi uliotokea tarehe 20 aprili 2006 pale kwenye makutano ya barabara ya MOROGORO na SAM NUJOMA jijini DAR ES SALAAM kwa fedha za benki ya NMB kuibiwa wakati zinasafirishwa kwenda mkoani MOROGORO (REJEA MAKALA YA UJAMBAZI MKUBWA UBUNGO MATAA)..

Sasa genge la MACHO MBAYA walikuwa wakishaiba magari nchini KENYA wana msogezea jambazi LYATUU jijini ARUSHA ayauze na hivyo hivyo magari yakiibiwa nchini TANZANIA yanasogezwa KENYA kwakina MACHO MBAYA kuuzwa, ni wanayavusha ili iwe ngumu kwa wamiliki walioibiwa au vyombo vya ulinzi na usalama kuyapata tena.

Kwenye nchi zote mbili za TANZANIA na KENYA kulikuwa na gereji ambazo kazi zake zilikuwa zinapokea magari ya uwizi na kuyabadilisha vitu muhimu kama rangi n.k ili yaingizwe sokoni na mmiliki wake akionyeshwa ndo hili gari lako anakataa sababu limebadilishwa na kuwa jipya machoni mwake.

Miaka ya nyuma kidogo uwizi wa magari ulishamiri sana na kuwa yanavushwa upande tofauti [KENYA au TANZANIA], sasa genge la MACHO MBAYA mshirika wao LYATUU hayupo ambaye ameuwawa mwaka 2006 katika zile operesheni za kutafuta majambazi wa UWIZI MKUBWA UBUNGO MATAA.

Kwahiyo wakina MACHO MBAYA wakaona hawawezi kukosa mshirika nchini TANZANIA na kuanza kumtafuta mtu wa kuaminika kama vile jambazi LYATUU, shida iliyokuwepo ni wakina MACHO MBAYA walikuwa wanataka mtu wa kuaminika sana kwaajili ya usalama wa shughuli zao za ujambazi nchini TANZANIA ila watu wanaofahamiana nao ni wengi sema ndo hawaaminiki sana.

Moja ya sababu zinazofelisha majambazi wengi na kuishia kukamatwa au kuuliwa ni washirika wao au wenyewe kwa wenyewe kukosa uaminifu hasa tamaa inapozalia baina yao na mwishoe wote wanaishi pabaya na kuwa wapotezaji.

Zoezi la kutafuta mshirika nchini TANZANIA lilifanyika kupitia wale watu wanaofahamiana nao ila ndo hawaamini kama vile walivyokuwa wanamuamini jambazi LYATUU ila inabidi waanze kuaminiana nao maana jambazi LYATUU kashauliwa hatarudi tena duniani na kikubwa ni kuwachambua na kuanza kuimarisha bondi [mahusiano] nao.

Washirika kutoka TANZANIA ambao waliona wanaweza kuchukua nafasi ya jambazi LYATUU ni bwana mdogo mmoja aitwaye SAMSON CHONJO aliyezaliwa mwaka 1981 na kipindi hicho mwaka huo 2007 alikuwa na umri wa miaka 26, ni kijana mdogo tu.

SAMSON CHONJO alikuwa ni mkazi wa NGULELO wilayani ARUMERU mkoani ARUSHA na kikazi alivyokuwa anatambulika ni dereva wa magari ya utalii na pia mwongoza watalii “TOUR GUIDE” sehemu za kutalii mkoani ARUSHA.

Mshirika mwingine wa pili alikuwa ni KALISTI JOSEPH KAMILI KISAMBU KANJE aliyezaliwa mwaka 1960 ambaye kipindi hicho mwaka huo 2007 alikuwa na umri wa miaka 47 na mkazi wa SANYA JUU wilayani SIHA mkoani KILIMANJARO akijishughulisha na biashara kwa kuwa mtu maarufu huko SIHA.

hawa wote walikuwa washirika wakuu wa genge la MACHO MBAYA na mawasiliano baina yao kuanza, na kitu kizuri sio wageni baina yao ni vile tu walikuwa hawaaminiki sana na genge la MACHO MBAYA na kama inavyojulikana uaminifu ndo nguzo kuu ya mafanikio yoyote kwenye shughuli zinazohusisha makundi na ikitokea mmojawapo ameharibu kwa kupoteza uaminifu basi kaua kundi nzima.

Mawasiliano baina ya genge la MACHO MBAYA na washirika wao nchini TANZANIA yalikuwa chanya kwa kukubaliana kufanya kazi na bwana KANJE kufurahishwa na jinsi genge la MACHO MBAYA lilivyojipanga akajitolea kuwa mfadhili wa shughuli za ujambazi zitakazofanywa na genge hilo la WAKENYA.

Bwana KANJE alicheza na fursa haraka kwa kupimia mbali kwamba akiwekeza kiasi fulani itajizalisha maradufu na kilichobakia kikawa ni genge la MACHO MBAYA kuhamia rasmi nchini TANZANIA na kazi ianze mara moja na kuna mambo makuu mawili genge la MACHO MBAYA lilikuwa limalizie hapo nchini KENYA ndo waanze safari.

Mambo hayo yalikuwa ni upatikanaji wa paspoti feki kwaajili ya MACHO MBAYA peke yake ambaye alikuwa kwenye orodha ya watu wanaotafutwa sana kwahiyo akitumia paspoti halali inayomtambulisha wasifu wake pamoja na picha yake basi atakuwa amekwisha.

Wanakundi wenzie ilikuwa haina shida sababu sio homa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya KENYA na hata hawajulikani kwa wenyewe kutembelea nyota ya MACHO MBAYA ambaye ndo kiongozi wao, na jambo lingine lilikuwa ni upatikanaji wa silaha pamoja na kuzivusha kuingia nchini TANZANIA.

Hayo mambo hawezi kuyafanya akiwa nchini TANZANIA na mara moja alianza kuyashughulikia kwa kutafuta paspoti feki kutoka kwa wataalamu wa kutengeneza nyaraka feki na kitu kizuri kipindi hicho hakukuwa na paspoti za kieletroniki ambazo zimesaidia sana kupunguza paspoti feki.

Suala la paspoti lilichukua muda mfupi sana likawa limekamilika na kuwa mkononi mwake MACHO MBAYA na suala la pili ambalo ni silaha likafuata kushughulikiwa na mfadhili bwana KANJE alianza ufadhili wake kuanzia hapo maana silaha hizo ndo zitakwenda kufanya kazi nchini TANZANIA.

Kwahiyo bwana KANJE alichotakiwa kufanya kama mfadhili akafanya na mfereji wa kuchukulia silaha ulikuwa ule ule wa SOMALIA na silaha zilikuwa za kivita kwa kuwepo silaha maarufu kama AK-47 pamoja na mabomu ambayo yalikuwa ya kurusha kwa mkono [mabomu ya kiazi].

Silaha zilikuwa mzigo mzito na nyongeza ya silaha zitaongezwa huko huko nchini TANZANIA kama zitahitajika kwa kutokea upungufu wa silaha, na silaha kuvushwa kuja nchini TANZANIA mpaka wa ROMBO ulionekana kuwa salama zaidi kuliko mipaka mingine ya KENYA na TANZANIA.

ROMBO ni wilaya ya mkoa wa KILIMANJARO kwahiyo mzigo wa silaha utaingilia mkoa wa KILIMANJARO na kuelekea mkoani ARUSHA ambako ndo MACHO MBAYA na genge lake walipachagua kuwa kitovu chao yani watahangaika mikoa mbalimbali kutekeleza ujambazi wao ila mwisho wa siku ARUSHA ndo kambi yao kuu kwa kupanga michoro yao ya ujambazi.

Faida ya mkoa wa ARUSHA kuwa kitovu chao ni ikitokea mambo yakivurugika rahisi kukimbia nchini TANZANIA kuelekea nyumbani kwao KENYA tofauti na kuweka kambi mikoa kama DAR ES SALAAM, DODOMA n.k lazima iwachukue muda na kuwa faida kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwadhibiti kwa kuwakamata au kuwaua.

Mpokeaji mzigo wa silaha ni wale washirika wao na kazi kama hii ndo faida ya kuwepo mwenyeji inaonekana na washirika wao walivyokwenda kupokea mzigo wa silaha walishangaa sana kuona mzigo mzito na kujua kweli wanaume wanakuja vitani na TANZANIA ijiandae nao.

Jambo la silaha kukamilika salama kwa kuvushwa na kufikishwa salama mkoani ARUSHA bila kujulikana ikawa imebaki genge la MACHO MBAYA kuanza safari kuja nchini TANZANIA na tarehe iliyopangwa ilikuwa 12 juni 2007 na hapo itakuwa imepita takribani miezi mitano toka ujambazi mkubwa wa mwisho nchini KENYA kufanywa na genge la MACHO MBAYA.

KENYA na TANZANIA wote hawajui genge la MACHO MBAYA linaelekea nchini TANZANIA na msako wa MACHO MBAYA nchini KENYA ulikuwa ukiendelea ila wanashindwa kumkamata ni anajua kuwakwepa vizuri ndo maana jina lake halitafutwa kwenye orodha ya majina ya majambazi wasumbufu kuwahi kutokea nchini humo.

KENYA waliunda mpaka kikosi maalumu ambacho kilikuwa na kazi moja tu ya kumkamata hai au mfu MACHO MBAYA na walikuwa wanausalama wabobezi ila alikuwa akiwapiga chenga ya mwili wao kikosi maalumu wakipata taarifa yuko sehemu fulani na wakifika haraka wanakuta ameshaondoka zamani.

MACHO MBAYA kama majambazi wengine wanahusishwa na imani za kishirikina kuwasaidia kuwa majambazi sugu walioshindikana kwa kila wanapokaribia kukamatwa kuna hisia zinawastua ambazo zinakuwa kama kuwashwa sehemu fulani, kubanwa na haja kubwa gafla n.k

Shida ni madai haya hayawezi kuthibitishwa ni yamekaa kiimani na bahati mbaya sana serikali zetu haziamini imani za kishirikina kwahiyo kitendo cha MACHO MBAYA kushindikana kukamatwa inahesabika anawazidi akili na sio uchawi unamsaidia.

Kipindi cha toka wazo la kwenda TANZANIA linazaliwa mpaka jambo la mwisho la mzigo wa silaha kuvushwa nchini TANZANIA kulitokea vifo vya wanagenge wa MACHO MBAYA katika ile operesheni ya jeshi la polisi kupambana na majambazi nchini humo.

Watu wake MACHO MBAYA muda mwingine walikuwa wakitekeleza ujambazi wao wenyewe na walikuwa huru kufanya hivyo sababu MACHO MBAYA kadri siku zilivyokuwa zikienda kasi yake ya kutafutwa ilikuwa ikiongezeka na kumfanya kupumzika kutekelea ujambazi akishughulikia mambo muhimu kabla hajahamia nchini TANZANIA.

Watu wake walikuwa hawako kwenye orodha ya watu wanaotafutwa sana kwahiyo waliendeleza ujambazi wa hapa na pale kuchangamsha miili yao isipoe pamoja na kupata fedha za kutanua mjini maana ndo ilikuwa kazi ya fedha zao hakuna cha kuwekeza biashara yoyote wala kujenga vibanda vya kujistiri.

Kwahiyo mpaka tarehe ya kusafiri kwenda nchini TANZANIA inafika MACHO MBAYA alikuwa na watu wake wawili tu ambao wako tayari kwenda naye ugenini na walikuwa ni PETER MBUGUA a.k.a NDUN’GU aliyezaliwa mwaka 1970 na mwaka huo 2007 alikuwa na miaka 37 na MICHAEL KIMANI PETER a.k.a KIM aliyezaliwa mwaka 1967 na mwaka huo 2007 alikuwa na miaka 40.

jambazi NDUN’GU na KIM wote ni wakazi wa jijini NAIROBI na walifahamiana na jambazi MACHO MBAYA kupitia kazi zao za kihalifu na kuamua kujiunga na genge la MACHO MBAYA, jambazi KIM kabla hajawa jambazi alikuwa dereva wa malori na baadae kuamua kuachana nayo kwa kuona inamchelewesha.

Hawa mapacha watatu kutoka KENYA ndo wanakwenda kusimamisha TANZANIA kwa kutangaza vita dhidi ya mali za WATANZANIA kuwa wanazitaka kwa nguvu na ukiwa mbishi hawacheki na wewe zaidi ya kukusafirisha kwa mola wako.

Tarehe 12 juni 2007 kufika MACHO MBAYA na genge lake walianza safari kuelekea nchini TANZANIA na walipanga kupitia mpaka maarufu wa NAMANGA ambao utawaingiza moja kwa moja nchini TANZANIA katika jiji lake la zuri na la kitalii yani ARUSHA.

Jambazi MACHO MBAYA sababu ya kuwa mtu anayetafutwa sana ilimpelekea muda wote wa safari mpaka hapo mpakani NAMANGA wanafika kuvalia koti lenye kofia “hood” na miwani nyeusi huku wenzie wamevalia kawaida kwa sura zao kuwa wazi hawana hofu yoyote.

Jambazi MACHO MBAYA na wenzie kukamilisha kila linalohitajika hapo mpakani NAMANGA kupitia ofisi za uhamiaji wakakutwa freshi na rasmi wakawa wamekanyaga ardhi ya TANZANIA, na MACHO MBAYA akavua koti lake na miwani nyeusi ili apumue kidogo na wakati huo mwenyeji wao bwana mdogo CHONJO alikuwa amefika mpakani hapo kuwapokea.

Genge la MACHO MBAYA na bwana mdogo CHONJO wakasalimiana na safari kuanza ambayo ilikuwa umbali wa kilomita 109.7, kuna mwendo kidogo mpaka kufika ARUSHA MJINI na njiani walikuwa wakipiga stori mbalimbali na moja ya stori ilikuwa mwenyeji wao kuwauliza wakina MACHO MBAYA kuhusu mzigo wa silaha mbona kuna mpaka mabomu.

MACHO MBAYA hakumjibu dogo kwa kuona anauliza maswali ya kijinga wakati wenzie wamejikoki kila idara sababu wanajua wamekuja vitani na hawatacheka na ngedere yoyote mbele yao atakayekuwa kiwingu, kama mtutu utamkosa basi bomu litamtawanya vipande vipande.

MACHO MBAYA alichofanya kwa mwenyeji wake kupotezea swali lake la kijinga ni kumuuliza ameshawatafutia watoto wazuri wa KIARUSHA wa kuburudika nao siku hiyo ili wapate joto murua la kukata baridi kali maana mwezi wa sita jijini ARUSHA ni kipindi cha baridi kali mwanzo mwisho.

Mwenyeji wake alimjibu MACHO MBAYA kuwa kwa hilo wasiwaze kabisa kila kitu kiko kwenye mstari mnyoofu ni wao tu kufurahia mabinti wazuri wa ARUSHA, na walipofika salama jijini ARUSHA wakina MACHO MBAYA walitaka kwanza kufika mahali mzigo wa silaha ulipohifadhiwa wauone ndo wapelekwe mahali pa kupumzika na kupata burudani za watoto wa KIARUSHA.

Wakina MACHO MBAYA kupitishwa kwenye maficho ya silaha hapo hapo ARUSHA MJINI na kuona ziko salama kama walivyozituma sasa wakawa tayari kuelekea kupumzika huku wakisubiri kesho yake kukuche na kazi iliyowaleta nchini TANZANIA kuianza mara moja.

Mwenyeji wao akawapeleka mpaka hotelini ambako tayari alishawasiliana na wadada poa [makahaba] kutangulia hotelini hapo katika vyumba husika ili wakina MACHO MBAYA wakifika waburudike, na hotelini watakaa kwa muda wakati nyumba inatafutwa ambayo ndo itakuwa kambi yao kuu.

Hotelini ni hatari kupanga mipango yao ya ujambazi, kuhifadhi fedha zao watakazoiba pamoja na silaha zao za kazi kwani wafanyakazi wa hoteli wanaweza kuwashtukia kwa kuona kitu kisicho cha kawaida vyumbani mwao na kutoa taarifa haraka kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kukamatwa.

Wakina MACHO MBAYA hotelini kufika wakakuta walichoahidiwa na mwenyeji wao na siku ikaisha vizuri kwao na tabia yakina MACHO MBAYA hasa kiongozi wao mwenyewe MACHO MBAYA kupenda sana wanawake itakuja kumgharimu mbeleni.

MACHO MBAYA alikuwa akijiona ni masta wa kucheza na mabinti za watu bila kumgharimu kama alivyokuwa anafanya nchini KENYA kwa mitego ya mabinti aliyojaribiwa kuwekewa na kikosi maalumu kuchomoka na kusahau kila mjanja ana wajanja wake.
Kosa moja goli moja na hicho ndo kitamfundisha kitu kizuri MACHO MBAYA na genge lake, kukucha asubuhi wakina MACHO MBAYA wakaanza kazi ambayo ilikuwa ni kuweka mikakati ya kazi yao ya ujambazi nchini TANZANIA huku mikoa lengwa ya kwanza ikiwa ARUSHA na KILIMANJARO.

Mikoa ya ARUSHA na KILIMANJARO ilichaguliwa kwanza sababu ya ukaribu wa kutorokea nchini KENYA endapo mambo yakaenda kombo, sababu itakuwa ndo mara yao ya kwanza kufanya ujambazi nchini TANZANIA kwahiyo lazima wapime maji kwa kijiti na sio mguu kuona kina chake.

Mikakati ikipangwa huku wakitegemea muongozo wa washirika wao, huku nyuma utafutwaji nyumba ulikuwa ukiendelea kwani ulianza hata kabla wakina MACHO MBAYA hawajafika nchini TANZANIA sema shida ilikuwa hakujapatikana nyumba sahihi kulingana na kazi itakayokwenda kufanyika humo ndani.

Nyumba ilitakiwa maeneo ya hadhi ya juu [ushuani] kwamba kila mtu yuko ndani kwake hakuna uswahili sijui mtoto wa jirani amekwenda kucheza kwa watu au mama amina anagonga hodi ya kuomba chumvi na karaha zingine za uswahilini, na hii yote ni kuepusha watu wa nje wasijue kiendeleacho ndani.

Sehemu zilizopendekezwa na washirika wa genge la MACHO MBAYA zilikuwa ni NJIRO na UZUNGUNI kwa huko kuaminika ni ushuani kwenyewe kila mtu kwenye geti lake hajui jirani yake anaishiji zaidi ya kupishana barabarani kwa kila mmoja akiwa kwenye usafiri wake.

Sasa nani aliyepewa kazi ya kutafuta nyumba ya kuishi wakina MACHO MBAYA…? Kuna binti mmoja aitwaye ELIZABETH ELIAS MSANZE a.k.a BELLA ambaye alizaliwa mwaka 1983 kwa kipindi hicho mwaka huo 2007 kuwa na miaka 24 ndiye ambaye alikuwa na jukumu la kutafuta nyumba watakayokaa wakina MACHO MBAYA.

ELIZABETH MSANZE naye alikuwa mshirika wa wakina MACHO MBAYA ambaye aliongezwa na washirika wa kwanza wa wakina MACHO MBAYA kwa binti huyu kutofahamika na kina MACHO MBAYA awali ila baada ya kufika nchini TANZANIA watamfahamu.

Binti huyu ndo alikuwa akizunguka na madalali kutafuta nyumba maeneo ya kishua ya UZUNGUNI na NJIRO, binti huyu akishapata nyumba atatakiwa kukodisha kwa jina feki la bibi FRANCIS URASSA ikimaanisha binti huyo ni mke wa mtu kwa mumewe kuitwa FRANCIS URASSA.

Binti ELIZABETH MSANZE atajazia kuwa mumewe FRANCIS URASSA ni mfanyabiashara wa magari na nyumba hiyo wanataka kutumia kama ofisi na kuonesha wako “serious” watalipa kodi ya miezi sita ya nyumba hiyo itakayopatikana ili kuaminisha yeye na mumewe ni wafanyabiashara wa magari.

Sasa binti ELIZABETH MSANZE ndo anahangaika na madalali kufanikisha jambo lake sababu anajua ukweli wa nyumba hiyo inakwenda kufanyiwa nini na hana shida kwa hilo sababu yeye anachoangalia ni fedha tu maisha yasogee, hawa ndo wale mabinti wadogo ambao mtu unashangaa mbona anapendeza kwa mavazi ya gharama na anakula bata lisilo kuwa na mwisho kumbe nyuma ya pazia ndo mambo kama haya.

Kisheria hapo ELIZABETH MSANZE naye ni jambazi bila kujalisha atashiriki moja kwa moja kuiba au laa na ikitokea mauaji pia naye ni muuaji bila kujalisha alishiriki mauaji hayo moja kwa moja au laa, na hizo ndo gharama za vijana kupenda maisha ya mkato endapo mambo yakaenda ndivyo sivyo ila mambo yakitulia kwenye reli ni raha tu na kuvimbia vijana wenzako ukiwa maeneo kama “KIDIMBWI”.

Siku mbili baada ya wakina MACHO MBAYA kufika nchini TANZANIA binti ELIZABETH MSANZE alishtuliwa kwa njia ya simu na dalali mmoja wa kike jijini ARUSHA aitwaye LILIAN MUSHI kuwa nyumba yenye sifa zile anazotaka imepatikana eneo la NJIRO kituoni KONTENA huku dalali akimwaga sifa kedekede kwa nyumba hiyo ili kuhakikisha mteja hachomoki maana walimuona ana hela.

Nyumba inayoongelewa na dalali MUSHI ni ghorofa moja ambayo ni mali ya bwana MAKOYE NGERERE ambaye ni mhandisi wa shirika la umeme TANZANIA yani TANESCO na hivyo karibuni alikuwa amehamishwa kikazi kutoka jijini ARUSHA na kupelekwa makao makuu ya TANESCO jijini DAR ES SALAAM.

Nyumba hiyo ilikuwa nzuri na ya kifahari, ELIZABETH MSANZE baada ya simu hiyo alijongea kwa dalali wake na wote kuelekea eneo la tukio kuona nyumba hiyo nzuri na walivyofika kwenye nyumba yenyewe wakamkuta mlinzi wa nyumba hiyo aitwaye HAMISI KIRONGA.

HAMISI KIRONGA aliwaruhusu kuona nyumba hiyo sababu alikuwa anajua inatakiwa kupangishwa na ELIZABETH MSANZE akaridhika na nyumba hiyo kwa kuwa na zile sifa ambazo wanazitaka wao kwaajili ya majambazi wao wageni wakina MACHO MBAYA.

ELIZABETH MSANZE akamwambia dalali kuwa anachukua nyumba hiyo na kutaka kujua bei yake na dalali alimwambia kwa mwezi kodi ni shilingi 450,000 na ELIZABETH MSANZE akaanza kushushana naye bei dalali mpaka kufikia shilingi 400,000 kwa mwezi na kuahidi atalipa kodi ya miezi sita.

Biashara ya nyumba ikawa imesha kwa kupatikana na kulipiwa, na mkataba rasmi wa nyumba hiyo ulisainiwa tarehe 17 juni 2007 na ndo siku ambayo kodi ilianza kuhesabiwa na majambazi wakina MACHO MBAYA kuhamia hapo siku hiyo hiyo ambayo ilikuwa jumapili huku mlinzi HAMISI KIRONGA akiambiwa huduma yake haitajiki tena hapo.

Muda wote wakina MACHO MBAYA toka wamefika nchini TANZANIA walikuwa wanapanga mikakati yao wakisubiria nyumba ipatikane ili wawe huru sasa kuanza tukio la kwanza la ujambazi wao ugenini na mikoa iliyopangwa kuanzwa kushambuliwa nao ilibaki ile ile ARUSHA na KILIMANJARO.

Mzigo wa silaha nao ukahamishwa nyumbani NJIRO hapo sababu usalama ni asilimia 100, jambazi MACHO MBAYA na genge lake wakaanza hatua ya kwanza ya ujambazi wao ambao ni kutafuta taasisi gani ya kifedha wanakwenda kuitenda na mkoa gani.

Wakina MACHO MBAYA wao hawataki ujambazi wa kitoto ule wa kuvamia majumba ya watu na kuiba mali na fedha kidogo zinazokuwepo kwenye nyumba husika, wao wanataka kwenda kuiba sehemu ambazo fedha ni za kutosha hakuna kubahatisha na sehemu hizo zinakuwa taasisi za kifedha kama mabenki, maduka ya kubadilisha fedha n.k

Huko ni uhakika sababu biashara yao ni fedha, wakina MACHO MBAYA na washirika wao wakaanza kutafuta taasisi ya kifedha katika mikoa ya ARUSHA na KILIMANJARO ambayo itakuwa na faida upande wao katika utekelezaji wa ujambazi wao wa kwanza nchini TANZANIA.

Baada ya kuzunguka huku na kule katika mikoa ya ARUSHA na KILIMANJARO na ikumbukwe mikoa hii ni majirani kwa kufuatana, waliweza kuangukia kwenye taasisi moja ya kifedha ambayo ni benki ya NMB [NATIONAL MICROFINANCE BANK] wilayani MWANGA mkoani KILIMANJARO.

Kwanini benki ya NMB wilayani MWANGA mkoani KILIMANJARO…? Kwanza ifahamike benki ya NMB wilayani MWANGA iko moja tu wilaya nzima na ipo maeneo ya MWANGA mjini karibu na barabara kuu ya mkoani ambayo inakwenda mikoa mingine.

Benki ya NMB wilayani MWANGA iko katika ghorofa ambayo ofisi za benki na makazi ya wafanyakazi wa benki yako hapo hapo yani chini ni benki juu makazi ya wafanyakazi wa benki, hapo hapo tayari ni kosa kubwa sana kwa benki au taasisi yoyote ya kifedha kufanya hivyo.

Taasisi yoyote ya kifedha ambayo biashara yake kuu ni fedha haitakiwi eneo moja kukaa na wafanyakazi ni hatari kwa usalama wa fedha katika taasisi hiyo na pia huchanganya walinzi husika wanaolinda benki hiyo na hili litakuja kujidhihirisha kupitia tukio la ujambazi wa wakina MACHO MBAYA.

Benki ya NMB wilayani MWANGA walikosea sana maana hata hao wafanyakazi wanaweza kufanya yao na kuwa hasara kubwa kwa benki ambayo ingewezekana kuzuilika, sasa kitendo cha benki na makazi ya wafanyakazi wake kuwa sehemu moja ilikuwa na faida kulingana na mchoro wa MACHO MBAYA utakavyokuwa yani mbuzi kafia kwa muuza supu.

Ukiachana na sababu kuu hiyo iliyofanya wakina MACHO MBAYA kuchagua benki ya NMB wilayani MWANGA mkoani KILIMANJARO kuna sababu zingine mbili zinatajwa ambazo ni KONSTEBO NATHANIEL MANYAMA na bibie SALOME MATEMU.

Sababu ya kwanza ambayo ni KONSTEBO NATHANIEL MANYAMA, huyu alikuwa polisi mwenye cheo cha KONSTEBO mkazi wa MONDULI mkoani ARUSHA na ameshawahi kuwa lindo katika benki ya NMB wilayani MWANGA mkoani KILIMANJARO.

KONSTEBO NATHANIEL MANYAMA anatajwa kuwa mshirika mwingine aliyeongezwa katika ujambazi huu kwa kusaidia mchoro wa tukio la ujambazi katika benki hiyo ya NMB sababu ya kuwa mzoefu na mazingira ya benki hiyo kwa kujua nje ndani usalama wa benki hiyo pamoja na njia ambazo majambazi watatumia kutorokea eneo la tukio.

Sababu KONSTEBO MANYAMA alionekana hana hatia na uhusika wa ujambazi huu kupitia mahakama basi kwa heshima yake na jeshi la polisi maana tayari alishatia doa jeshi hilo hatutamchimba ila tukiachana na mambo ya sheria na mahakama kwa kutumia mahakama zetu za vichwa vyetu basi huyu askari tungemsukumia kwenye kundi moja na wakina MACHO MBAYA.

Tunasema mawakili wake walifanya kazi kubwa na nzuri kwa kucheza vizuri na sheria, sawa tu na vile ACP ABDALLAH ZOMBE jinsi mawakili wake walivyofanya kazi kubwa na nzuri kwa kucheza vizuri na sheria mwishoe naye akaonekana hana hatia.

Sababu ya pili ambayo ni bibie SALOME MATEMU ambaye huyu ni mfanyakazi wa benki ya NMB wilayani MWANGA mwenye cheo cha meneja operesheni naye anatajwa kuwa mshirika wa ujambazi huu wa benki ya NMB MWANGA kwa kuongezwa katika washirika wa genge la MACHO MBAYA.

Meneja operesheni SALOME MATEMU ndiye kiongozi wa kuba ya kuhifadhia fedha yani funguo na ruhusa ilikuwa katika mamlaka yake na kwa mustakabali huo alikuwa akijua kuba ya NMB MWANGA ina nini kwa kiasi gani, kuba ni sehemu ambayo inahifadhi vitu vya thamani vya benki/taasisi za kifedha kama fedha, madini n.k kutoka kwa wateja wao.

Meneja operesheni SALOME MATEU anatajwa kusaidia mchoro wakina MACHO MBAYA kuhusu benki ya NMB MWANGA na sababu alikuwa akiijua nje ndani akawasaidia, ila huyu bibie MATEU ni kama KONSTEBO MANYAMA alionekana hana hatia yoyote mbele ya mahakama ila kwa mahakama ya vichwa vyetu tusingemuacha tungemsukumia huko katika kundi la kina MACHO MBAYA.

Meneja operesheni SALOME MATEU kwa heshima yake na benki aliyokuwa anafanyia kazi yani NMB ambayo tayari alishaitia doa kwa namna ushahidi ulivyokuwa ukimtafutana na uhusika wa ujambazi huu naye hatutamchimba.

Sasa sababu zote hizo zilichangia MACHO MBAYA na genge lake kuchagua benki ya NMB MWANGA kufanya tukio la kwanza la ujambazi nchini TANZANIA na kwa kuwa benki ishapatikana kilichofuata sasa ni mchoro wa ujambazi kuandaliwa ili utekelezaji kuanza mara moja.

Wakati mambo ya mchoro wa ujambazi benki ya NMB unaanza yule binti ELIZABETH MSANZE alikuwa na ndugu zake watatu ambao ni DEVOTHA ELIAS MSANZE, JULIANA ELIAS MSANZE na NTABASILE ELIAS MSANZE na wote hawa kiumri ni wakubwa zaidi ya ELIZABETH ELIAS MSANZE.

ELIZABETH MSANZE na ndugu zake hao wakawa wapenzi wa genge la MACHO MBAYA na washirika wake na hili lilikuwa kosa la kwanza upande wakina MACHO MBAYA kwa kupindisha sheria yao waliojiwekea wenyewe toka wakiwa nchini KENYA.

Wakina MACHO MBAYA sheria yao waliojiwekea wenyewe ni kutokuwa na mpenzi wa kudumu hata siku mbili tatu yani wao walikuwa wakiishi katika ule msemo wa vijana wa mjini “hit n run” na hii iliwasaidia sana kukwepa mitego ya kile kikosi maalumu cha polisi nchini KENYA.

Wakina MACHO MBAYA waligundulika udhaifu wao ni mabinti na kikosi maalumu kutumia udhaifu huo kama wataweza kuwakamata ila mpaka wanahamia nchini TANZANIA walishindwa kuwakamata kwa mtego huo ila sasa nchini TANZANIA wanakwenda kuharibu kila kitu kwa kujisahau.

Maana kwao hao ndugu mapenzi yao yatakuwa “hit n stay” na makosa yake yatakuja kuonekana mbele, na katika kosa la kwanza hilo ndani yake kuna kosa lingine dogo ambalo lilikiuka sheria walizojiwekea wao wenyewe na kosa hilo ni kufanyia mambo yao humo humo ndani ya nyumba waliyopangisha NJIRO.

Wakina MACHO MBAYA wakiwa nchini KENYA walikuwa hawafanyi hivi kwa wanawake wanaokula nao raha sababu ni hatari kwa wanawake hao kubanwa au kuwa wametumwa na polisi kuwachunguza kuwaleta vyombo vya ulinzi na usalama wanapoishi na ikumbukwe wakina MACHO MBAYA hapo nyumba waliyokodisha ndo nyumbani na makao makuu yao kwa wakati wote watakaokuwa nchini TANZANIA.

Hao ndugu wakina MASANZE wakina MACHO MBAYA walitakiwa kula nao raha nje ya nyumba ya NJIRO ili wasijue wao wanaishi wapi ingawa kwa upande wa ELIZABETH MSANZE isingewezekana sababu ndiye aliyetafuta nyumba hiyo.

Mwisho wa siku kosa kubwa la kujihusisha nao kimapenzi ndo lilikuwa la kujiepusha nalo ili kusiwepo hilo kosa dogo ndani yake la kuwakaribisha hapo nyumbani NJIRO na binti ELIZABETH wangebaki washirika tu kwa kuheshimana kama walivyokuwa wanaheshimiana na washirika wao wengine.

Waswahili wanasema “NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE”, kwahiyo wakina MACHO MBAYA wakiendelea kula burudani na hao mabinti uanzaji wa mchoro nao ulianza na walikuwa wakishuhudia na kusikia kila kitu yani wakina MACHO MBAYA walijisahau sana.

Hao ndugu mpaka silaha walikuwa wanaziona na kuzichezea kama midoli, vichwa vikaanza kusuguliwa na wakina MACHO MBAYA huku wakipata ushirikiano wa washirika wao pale wanapohitaji taarifa zaidi ili watoe mchoro wenyewe kulingana na madhaifu ya benki ya NMB MWANGA.

Baada ya siku kadhaa ambapo ilikuwa mwanzoni kabisa mwa mwezi julai 2007 mchoro mzima ulikuwa umekamilika na kubakia utekelezaji tu na ulikuwa mchoro mzuri sana ambao ulionesha kweli wakina MACHO MBAYA walikuwa wamekuja kufanya kazi nchini TANZANIA.

No comments

Powered by Blogger.